27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BILLICANAS YA MBOWE YAZAMISHWA RASMI

nhc

NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.

Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.

Gazeti hili lilishuhudia ubomoaji huo ukiwa katika hatua za awali na baadhi ya vijana walionekana wakianza kuondoa vioo na vigae vilivyoezekwa katika jengo hilo wakiwa chini ya usimamizi wa walinzi.

Hata hivyo, walipoulizwa watu waliokuwa wakisimamia katika eneo hilo walidai kuwa ubomoaji huo ni wa kawaida na ulipangwa kufanyika muda mrefu na endapo waandishi watahitaji maelezo wawasiliane na uogozi wa NHC.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alikiri shirika hilo kuanza kubomoa jengo hilo na kusisitiza kuwa ubomoaji huo utadumu kwa muda wa siku tatu.

“Nipo likizo lakini najua kama jengo linabomolewa, ubomoaji huo umeanza leo (jana) na utamalizimika Jumapili (kesho),” alisema Mchechu.

Alipoulizwa aina ya uwekezaji uliopangwa kufanywa na NHC katika eneo hilo baada ya ubomoaji huo aliahidi kutoa maelezo hayo keshokutwa.

“Naomba tu univumilie leo (jana), jua tu tunabomoa jengo maelezo ya kinajengwa nini na kwa matumizi gani nitayatoa Jumatatu (keshokutwa), naomba tuonane siku hiyo utapata maelezo yote,” alisema Mchechu.

Mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa  thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe siku 14  kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.

Mpango huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.

Mwanasenga alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo na masuala ya siasa.

Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.

Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.

Pia Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.

Kuhusu kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.

Katika shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.

Kabla ya Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo, Mchechu, alikaririwa akisema kuwa NHC inazidai taasisi za umma na watu binafsi jumla ya Sh bilioni 15 na kutoa notisi ya siku 60 kwa wadaiwa hao.

Mbali ya Bilicanas, Mchechu alitaja  wadaiwa wengine kuwa ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh bilioni mbili, Benki ya Azania inadaiwa Sh milioni 161 na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa inadaiwa Sh milioni 631.

Wadaiwa wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (Sh bilioni moja).

Desemba 3, mwaka jana Mkurugenzi wa Mikoa na Utawala wa NHC, Raymond Mndolwa, alikaririwa na vyombo vya habari akisema baada ya kutoa notisi   shirika hilo lilikusanya Sh bilioni 5.9 kati ya Sh bilioni 9.3 ambalo ni deni la Serikali kupitia wizara na taasisi mbalimbali, huku Sh bilioni 2.5 zikikusanywa kutoka kwa wadaiwa binafsi ambao awali walikuwa wanadaiwa Sh bilioni nne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles