23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

22 WATIBIWA MFUMO UMEME WA MOYO JKCI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM                 |              


WAGONJWA 22 waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo yatokanayo na mfumo wa umeme wa moyo, wamefanyiwa upasuaji mdogo na kuwekewa vifaa maalumu vya kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge.

Alisema matibabu hayo yamefanyika hospitalini hapo katika kambi maalumu ya siku saba ya kutibu matatizo ya moyo kwa upasuaji wa bila kufungua kifua (catheterization) kwa kutumia mtambo maalumu wa cathlab.

Dk. Kisenge, alisema madaktari wa JKCI wamefanya kambi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa nchini Marekani kutoka Shirika la Madaktari Afrika.

“Kambi hii ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yao yalikuwa chini kwa kiwango cha asilimia 50 kwa dakika, tumewawekea kifaa maalumu kinachosaidia mapigo ya moyo kuongezeka (pacemaker),” alisema.

Alisema kazi ya kifaa hicho ni kuwasaidia wagonjwa wasipoteze maisha ghafla.

“Mara nyingi wagonjwa wenye matatizo ya mapigo ya moyo ambayo yako chini hufa vifo vya ghafla,” alisema.

Alisema upasuaji huo ulienda vizuri na kwa ufanisi mkubwa na kwamba pia wapo wagonjwa wengine waliopandikizwa kifaa cha ICD (Implantable Cardioverter Defibrillator), hasa wale ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimia 30.

Naye, Profesa Matthew Sackett, kutoka Shirika la Madaktari Afrika, alisema kambi hiyo ilienda sambamba na utoaji wa elimu kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya.

“Imekuwa ni wiki ya mafanikio kwetu, tumetibu wagonjwa na nimewapa elimu ya namna ya kumuwekea mgonjwa kifaa cha  ICD kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya, nitakuwa nakuja kuwapa elimu kila nitakapopata nafasi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles