24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UFISADI WA KIHISTORIA

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola

Na VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), imevunja ukimya na kumtaja raia wa Tanzania mwenye asili ya Asia, Mohamed Yusuph Ally, kuwa ndiye kinara wa kutengeneza stakabadhi za kielektroniki kupitia mashine za EFD’s, huku wakimtaka kurejesha fedha alizoiba kwa hiyari yake.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kueleza umma kwamba mfanyabiashara huyo amekuwa akifanya miamala ya fedha inayofikia Sh milioni 7 hadi 8 kwa kila dakika moja.

Pamoja na hatua hiyo, Takukuru pia imebaini zaidi ya kampuni 300 zimekuwa zikihusika katika mchezo huo mchafu, na kwa pamoja zimetakiwa kulipa takribani zaidi ya Sh bilioni 30, ambazo zinaelezwa zimeibwa kupitia mtindo huo wa kudurufu stakabadhi bandia zenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wakizungumza kwa pamoja na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Kamishna Valentino Mlowola na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, walieleza jinsi kampuni hizo feki zilivyoiibia Serikali kupitia stakabadhi za mfumo wa kielektroniki (EFD’s).

Kamishna Kidata, alisema kampuni hizo zimekuwa zikinunua stakabadhi za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za kielektroniki ambazo hazijasajiliwa  na kuzitumia na kisha kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwapo na bidhaa au stakabadhi halali iliyouzwa au kutolewa na muhusika.

Kutokana na hali hiyo, alisema TRA kwa kushirikiana na Takukuru bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kampuni zote zinazojihusisha na mchezo huo mchafu wa kuiibia Serikali.

Mtendaji huyo wa TRA alisema hadi sasa tayari wamezibaini kampuni nne ambazo zimekuwa zikijihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huo tangu mwaka 2010 hadi 2014 na kupoteza mapato ya Serikali kiasi cha Sh bilioni 29.2.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Skol Building Material Ltd, ambayo imebainika tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa VAT ya Sh bilioni 5.4 na kodi  ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 10.9, hivyo kudaiwa jumla ya Sh bilioni 16 kwa kipindi hicho.

Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Ltd, ambayo alisema tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikuwahi kulipa VAT ya jumla ya Sh bilioni 5 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 4 ambayo ni jumla ya kodi inayodaiwa kufikia Sh bilioni 9.

“Kampuni nyingine ni A. M Trailer Manufacturers Ltd ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014 haikuwahi kulipa VAT ya Sh bilioni 6 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 1 ambayo jumla ya fedha inazotakiwa kurejesha ni Sh bilioni 1.7.

“Baada ya kubaini ukwepaji kodi wa makampuni haya, TRA kwa kushirikiana na Takukuru inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na baada ya uchunguzi kukamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi,’’ alisema Kidata.

Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa wafanyabiashara kutojihusisha na kununua stakabadhi bandia, na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka imejizatiti kuendelea kuwabaini wakwepa kodi wote.

Kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa TRA kujihusisha na mtandao huo wa kudurufu mfumo wa kukwepa kodi na kuiibia Serikali mapato, alisema wanaendelea na uchunguzi na kama wapo nao wanachukuliwa hatua za kisheria.

“Ni kweli mashine za EFD’s huwa zinaletwa na kampuni binafsi kisha TRA tunazichukua na kuziingiza katika mfumo wetu ambao tumeuboresha hivi sasa.

“Ndiyo maana hizi EFD’s feki ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo huu, tuna uwezo wa kuzibaini kwa sababu zinakuwa ‘detected’, hivyo tunachunguza kujua kama wapo maofisa wa TRA ambao walihusika katika suala hili,” alisema Kidata.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TRA, Kamishna Mlowola, alisema uchunguzi bado unaendela kwa kampuni 300 ambazo zimetakiwa kulipa fedha hizo na wakishindwa watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na hali hiyo, alisema mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) pamoja na TRA.

Mtandao mpana

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa mtandao wa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakiibia Serikali, upo kwa makampuni zaidi ya 20,000 ambazo zimekuwa zikiendesha mchezo huo mchafu tangu 2010.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa wiki moja sasa vyombo vya dola vimekuwa vikipambana na mtandao huo ambapo inaelezwa kuwa vinara hao tayari wapo katika mikono salama.

“Hadi sasa tayari Serikali imeshakusanya mabilioni ya fedha na mtandao huu umefanya kazi kwa muda wa miaka mitano. Na ambao wamekamatwa hadi sasa kuna wafanyabiashara wawili wenye asili ya Kiasia pamoja na Mtanzania mmoja ambaye ndiye amekuwa kinara wa kuunganisha mashine hizo kwa kutumia wataalamu kutoka nje.

“Si hivyo tu, tangu wakati huo walikuwa wakishirikiana na watendaji wa ngazi za juu serikalini pamoja na wale wa TRA, na hawa ndio walikuwa wameomba zabuni kwa njia za ujanja za kuingiza mashine za EFD’s,” alisema mtoa habari wetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles