24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

1,065 mikononi mwa Kamanda Sirro

Kamishna Simon Sirro
Kamishna Simon Sirro

Na Asifiwe George, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanya operesheni katika maeneo mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu 1,065 kwa makosa mbalimbali likiwemo la unyang’anyi wa kutumia nguvu pamoja na silaha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema vijana hao pia wamekuwa wakifanya wizi kutoka maungoni, wengine kupiga debe, watengenezaji na wanywaji wa pombe haramu ya gongo, kundi la vijana wanaovunja nyumba za watu kwa kutumia silaha za jadi maarufu ‘kumi nje kumi ndani’ na wacheza kamari.

Alisema vitu vilivyokamatwa na jeshi hilo ni gongo lita 952 na mitambo mitatu ya kutengenezea pombe hiyo, bangi puli 277, kete 210, misokoto 144, kucheza kamari.

Katika tukio lingine, Julai 21 mwaka huu saa 10:00 jioni katika eneo la Kawe Jangwani Sea Breeze, askari walifanikiwa kukamata silaha aina ya Gobole yenye namba za usajili HD 201-2014 ikiwa imetelekezwa maeneo hayo na watu wasiofahamika.

Alisema silaha hiyo ilipatikana baada ya askari kupata taarifa kutoka kwa raia wema, waliosema kuna mtu wanamhisi ana silaha ndipo askari walifika eneo husika na kukuta silaha hiyo imetelekezwa kwenye eneo hilo.

Kamanda Sirro alisema msako wa kuwatafuta watuhumiwa bado unaendelea.

Pia Kamanda Sirro alisema jeshi hilo limewakamata vijana watatu kwa kosa la uporaji wa simu kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kinondoni.

Aliwataja vijana hao kuwa ni Richard Augustine (18) ambaye alikamatwa eneo la Coco Beach akiwa na simu aina ya Sumsung Duos yenye thamani ya Sh 500,000 na mtuhumiwa mwingine, Abdalah Chande (36), aliyekamatwa eneo la Magomeni Mapipa akiwa na simu 11 za aina mbalimbali zinazodaiwa kuwa ni za wizi.

Alisema mtuhumiwa mwingine, Abdalah Saidi (22), alikamatwa katika eneo la Mburahati Madoto akiwa na pikipiki MC 766 BFE aina ya Boxer nyeusi inayotumika kwa uporaji wa simu maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kinondoni.

“Uchunguzi wetu wa awali umebaini watuhumiwa wote watatu wanafahamiana na kukiri kufanya matukio ya wizi wa simu, upelelezi unaendelea na ukikamilika watuhumiwa watapelekwa mahakamani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles