28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto wanaozaliwa wakipungua, wazee waongezeka

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA

UTAFITI mpya umedai kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa imekuwa ikipungua duniani kote kwa kiwango kikubwa na kusababisha pengo la idadi ya watu katika baadhi ya mataifa hasa ya Magharibi.

Utafiti huo umebainisha kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa imeshuka na wengine hushindwa kuzaliwa kutokana na mimba kuharibika.

Watafiti wamedai matokeo ya utafiti huo yaliwashangaza na ni hali, ambayo  imesababisha jamii kuwa na wazee wengi zaidi ya wajukuu.

Utafiti ambao ulichapishwa katika Jarida la Sayansi la Lancet mwishoni mwa mwaka jana, ulifuatilia mwenendo wa kila nchi kuanzia mwaka 1950 hadi 2017.

Kwa mujibu wa utafiti mwaka 1950, wanawake walikuwa na wastani wa uzazi wa watoto watano, kiwango ambacho kufikia mwaka juzi kilishuka hadi wastani wa watoto wawili.

Lakini hali hiyo ina utofauti mkubwa kati ya nchi na nchi. Kwa mfano kiwango cha watoto wanaozaliwa nchini Niger ni watoto saba wakati kwenye fukwe za Bahari ya Mediterania, wastani wa mwanamke kujifungua ni mtoto mmoja.

Kipindi ambacho idadi ya watoto wanaozaliwa inapungua kwa wastani wa watoto wawili basi idadi ya watu pia huathirika na taifa kujikuta likiwa na wazee wengi.

Takwimu ya mimba zinazoharibika pamoja vifo vya watoto wachanga vimeongezeka pia kwa mujibu wa utafiti huo mkubwa.

Mwanzoni mwa utafiti huo mwaka 1950, hakukuwa na taifa hata moja ambalo lilikumbana na changamoto ya kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, hali ambayo hata hivyo imekuwa ikibadilika mwaka hadi mwaka.

Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Tathmini mjini Washington, Marekani, Profesa Christopher Murray, alisema ” tumefikia mahali ambapo nusu ya mataifa yana upungufu wa watoto wanaozaliwa dhidi ya waliopo”.

“Hivyo kama hakuna hatua, ambayo itachukuliwa basi idadi ya watu itapungua katika hayo mataifa na kuathiri nguvu kazi.”alionya.

Aliongeza kwa kudai mabadiliko haya yamewashangaza wengi kwa kupungua kwa idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa kote duniani, kiwango ambacho alisema si tu ni kikubwa bali pia cha kustaajabisha. 

Nchi ambazo zimeendelea zaidi kiuchumi zikiwemo nchi zilizopo barani Ulaya, Marekani, Korea Kusini na Australia kuna kiwango kidogo cha watoto wanaozaliwa.

Lakini hilo halimaanishi idadi ya watu wanaoishi katika mataifa hayo imepungua kutokana na upungufu huo kuonekana kuzibwa kwa namna nyingine.

Kwa sasa bado kiwango cha idadi ya watu imechanganyika na wanaozaliwa na kufa pamoja na wahamiaji.

Lakini Profesa Murray anasema kwamba hali hii inapelekea dunia kufikia hatua ambayo jamii itaanza kuathirika kwa kupungua kwa idadi ya watu.

Nusu ya mataifa duniani bado wanawake wanazaa watoto wanaotosheleza mahitaji yao lakini kadiri nchi zinavyokua kiuchumi idadi ya wanaozaliwa pia inapungua.

Kupungua kwa kiwango cha watoto wanaozaliwa hakutokani na watu kushindwa kuwa na nguvu ya kuzaa au jambo lolote linalohusisha na uzazi bali kutokana na sababu kadhaa ikiwamo familia kupanga watoto wachache, upatikanaji wa dawa za uzazi wa mpango na wanawake kujikita katika elimu na kazi zaidi.

Kutokana na sababu hizo, mataifa yanayokabiliwa na upungufu wa uzazi, yanalazimika kugeukia wahamiaji ili kuziba pengo la upungufu wa nguvu kazi.

Dk. George Leeson, Mkurugenzi wa Chuo cha Oxford nchini Uingereza anasema kwamba hali hiyo si jambo baya ilimradi jamii yote haiathiriki na kiwango cha mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa.

Amesema kiwango hicho kimeathiri maisha ya kila mmoja na ukiangalia watu mitaani , kwenye makazi yao na foleni za barabarani .

“Matumizi yao yanategemea kiwango cha watu kilichopo. Kila kitu ambacho tunapanga kinatokana na idadi ya kiwango cha watu lakini vilevile vile ,umri wao pia huwa unaleta mabadiliko.’

Mtaalamu huyo anafikiri kwamba maeneo ya kazi yanaweza kubadilika na hata kuwataka watu wastaafu kufanya kazi wakiwa juu ya umri wa miaka 68 ambao ndio kiwango cha mwisho nchini Uingereza.

Nchi ambazo zimeathirika zitahitajika kuongeza idadi ya wahamiaji na kuanzisha sera mpya ili kuwahamasisha wanawake kuzaa watoto zaidi ambapo mara nyingi inashindikana.

Mwandishi wa ripoti hiyo, Profesa Murray amebaini kwamba kutakuwa na watoto wachache na watu wengi ambao wana umri juu ya 65 hivyo itawawia vigumu kukabiliana na mabadiliko haya duniani.

Ukifikiria juu ya matokeo ya kiuchumi na kijamii ya namna ambavyo kuna bibi na babu wengi zaidi ya wajukuu, alisema na kuongeza;

“Nadhani Japan inafahamu kuwa ina upungufu wa idadi kubwa ya kiwango cha watu wanaozaliwa. Lakini nchi nyingi zilizopo kaskazini hazitaathirika kwa sababu ya idadi ya watu waliopungua itafidiwa na wahamiaji.”

Ingawa kiwango cha watu duniani, hakuna suluhisho la uhamiaji. Mabadiliko hayo yanaweza kuathiri jamii, vilevile kutakuwa na mafanikio ya kimazingira ambayo yataleta manufaa katika jamii yetu.

China ina kiwango kikubwa cha ongezeko la watu tangu mwaka 1950, ambapo inakadiriwa kuwa nusu bilioni ya kiwango cha watu wote.

Lakini bado wanakumbana na changamoto ya kiwango cha watu wanaozaliwa, hali iliyosababisha waelekee kwenye sera ya kuwa na mtoto mmoja tu.

Sababu za nchi zinazoendelea kuhitaji kuongeza idadi ya watu wanaozaliwa ni kwa sababu si watoto wote huwa wanaweza kuishi kufikia utu wazima na watoto wengi ni wavulana zaidi ya wasichana.

Hata hivyo suala la wahamiaji linaendelea kuzusha mfarakano katika jamii hasa katika mataifa ya Magharibi, ambalo limeigawa mara mbili.

Kwa mfano nchini Ujerumani, taifa kubwa zaidi kiuchumi barani humo, uchunguzi uliochapishwa hivi karibuni umebainisha Ujerumani inahitaji wahamiaji ili kuziba kupungua kwa kiwango cha uzazi.

Gazeti la “Nürnberger Nachrichten” limemulika uchunguzi huo na kuandika:”Tunahitaji wahamiaji 260.000 kwa mwaka, zaidi ya nusu ni wa kutoka nchi ambazo si wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Hayo yametajwa na wataalamu katika ripoti yao iliyochapishwa hivi punde. Hilo lakini wananchi ambao baadhi yao bado wana kihoro kufuatia wimbi la wahamiaji la mwaka 2015 ikiwamo wanaosababisha vitendo vya kigaidi vilivyoliza wengi, wanabidi waelezwe.

Hata hivyo, katika harakati za kuziba pengo la upungufu wa watoto wanaozaliwa, ambapo wahamiaji huonwa kama suluhu, nchini Hungary wameanzisha mkakati wa kuzaa watoto wengi.

Katika hatua hizo zinazochukuliwa wanandoa vijana watakuwa wanapewa mkopo usio na riba wa dola 26,000 ambao utafutwa watakapofikisha watoto watatu.

Wanasiasa wa mrengo wa kulia nchini humo wamekuwa wakipinga uhamiaji unaofanywa hasa kutoka jamii za Waislamu.

Idadi ya watu nchini Hungary imekuwa ikipungua kwa 32,000 kwa mwaka na wanawake nchini humo wana watoto wachache kushinda wastani wa Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban amesema imesema kwa nchi za magharibi jibu la kupungua kwa watoto wanaozaliwa Ulaya ni Wahamiaji lakini watu wa Hungary wanafikiri tofauti, hatuhitaji wahamiaji, tunataka watoto wa Hungary.” alisema.

Waziri Mkuu huyo wa Hungary amekuwa akichukua hatua kali dhidi ya wahamiaji, hali ambayo mara kwa mara imefanya kutofautiana na wenzake wa Ulaya.

Ufaransa ni nchi inayoongoza kwa mwanamke kuzaa watoto wengi nchi za Umoja wa Ulaya kwa wastani wa 1.96 huku Hispania ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha 1.33.

Niger nchi iliyoko Afrika Magharibi ndiyo inayoongoza kwa mwananmke kuzaa watoto wengi duniani kwa watoto 7.24 kwa mwanamke mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles