24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wasanii 2019 ongezeni ubunifu zaidi

NA JOHANES RESPICHIUS

MWAKA 2018 ni mwaka ambao umekuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya sanaa hapa Tanzania, kwa sababu kipindi hiki ndiyo tumeshuhudia tasnia ya muziki, filamu na nyingine zikikua kwa kiasi kikubwa.

Zikiwa zimebaki siku mbili kuanza mwaka mpya, jitihada hizo zinapaswa kuendelea ili kuinua sanaa yetu katika hatua nyingine kubwa ya maendeleo, kila kitu kinawezekana kama wasanii wakifanya kazi zao kwa ubunifu na ubora unaotakiwa.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili, ubunifu ni matumizi ya njia bora zaidi zinazokidhi kutatua changamoto mpya, changamoto ambazo tayari zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi bado au zile zilizopo kwenye soko au jamii kwa kipindi husika.

Muktadha huo unatimilika pale ambapo bidhaa, huduma, teknolojia, mpangilio wa biashara au  njia yoyote inayoweza kutatua changamoto husika katika jamii ni adimu kuipata katika masoko mbalimbali ya bidhaa duniani.

Katika nchi zilizoendelea dhana ya ubunifu kwenye sanaa yoyote inaangaliwa zaidi, jambo ambalo limekuwa likiwawezesha kupiga hatua katika soko la dunia.

Nchi kama Marekani, India, China, Uingereza na nyingine sanaa ni moja ya sekta zinazowaingizia mapato makubwa wasanii na Serikali zao kutokana na kazi hizo kutengenezwa kibunifu na kwa ubora unaokidhi.

Kwa nchi za Afrika kazi za sanaa kama muziki, filamu, sanaa za ubunifu na maonyesho zimeshindwa kuendelea kutokana na kutokidhi vigezo vya ubora vya kimataifa.

Msanii wa muziki wa hip hop, Mtalemwa Jason ‘Nash Mc’, juzi kupitia ukurasa wake alijaribu kueleza aina moja ya ubunifu ambao msanii anapaswa kuwa nao hususan anapokuwa anatumbuiza kwenye majukwaa mbalimbali.

Nimelipenda wazo la Nash Mc kwa sababu ametumia uwanja huo kuwataka wasanii katika mwaka 2019 waache kugandamizia nyimbo zao wanapokuwa jukwaani na badala yake wawe wahalisia kwa kuimba moja kwa moja.   

Nash anasema utakuta kipaza sauti kipo Tegeta mdomo upo Buza, halafu msanii unaruka ruka jukwaani na kesho yake wanaanza kusifiana kuwa fulani alifunika sana kwenye onyesho kwa kuwa wote wanafanya ujinga mmoja.

Ukuaji wa muziki unaendana na viwango vya wasanii katika ufanyaji wa maonesho ya jukwaani ndipo maana kwa upande wake ameamua kuacha kabisa kutumbuiza wimbo ambao mashairi yake ameyasahau kuliko kuwaongopea mashabiki.

Hiyo ni aina moja tu ya ubunifu, lakini kuna vitu vingi ambavyo wasanii wanapaswa kuvifanya katika kazi zao ili mwaka ujao uwe wa mafanikio zaidi ya 2018, tunahitaji wasanii waonyeshe vitu tofauti zaidi.

NUKUU

“Ukitaka kumwelewa mtu angalia vile anavyowachukulia wale ambao anajua hata iweje hawawezi kumsaidia kitu chochote,”

Nikki wa Pili

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles