31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UVCCM watoa msimamo kuhusu Lowassa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MWANGWI wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kurejea CCM umeendelea kutikisa ndani na nje ya chama hicho tawala, huku Umoja wa Vijana (UVCCM), ukitoa msimamo kuhusu hatua hiyo.

UVCCM imewajia juu watu wanaomsema vibaya Lowassa huku wakihoji wanaofanya hivyo baadhi yao wapo ndani ya CCM na kuhoji usafi wao.

Lowassa alitangaza kurejea CCM Machi 1, mwaka huu akitoka Chadema ambako alijiunga Julai 27, 2015 baada ya kuridhiwa na Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani na baadaye kumtangaza kuwa mgombea urais akipeperusha bendera ya Ukawa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Lowassa aliyeweka rekodi ya kuwa mgombea urais wa upinzani aliyepata kura nyingi zaidi ya milioni sita, Machi 9, mwaka huu alikabidhiwa kadi rasmi ya CCM nyumbani kwao wilayani Monduli mkoani Arusha kwa shamrashamra.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James, alishangazwa na baadhi ya watu wanaomsema vibaya Lowassa wakati wao si wasafi.

Alisema mara baada ya uhakiki wa mali za CCM, kuna majina ya baadhi ya viongozi wameonekana kutafuna mali za chama, lakini bado hadi leo wamevumiliwa jambo ambalo nao wanatakiwa kufanya hivyo kwa Lowassa.

 “Kuna viongozi wamevumiliwa kwa mambo mengi ndani ya CCM, tumefanya uhakiki wa mali za chama nchi nzima, ukifungua kabrasha la uhakiki wa mali ni majina ya watu je, tumewapeleka mahakama gani?

“Kama nyinyi mmevumiliwa kwa hayo, kwanini Lowassa asivumiliwe? Sisi mtu akifanya kosa na kakiri kosa na akawa tayari kukiri kosa hatuoni dhambi ya kuanza upya.

“Nani asiye na dhambi hapa anyooshe mkono, nani msafi hapa anyooshe mkono? Ndugu zangu mkosefu wa ovyo ni yule anayekosa halafu hataki kurekebishwa, lakini mkosaji wa kweli ni yule ambaye anakosa, anaomba radhi na anachukua hatua za kuomba radhi.

“Nani asiyejua kwamba Lowassa tulimtuhumu kwa haya na yale na mengine amekiri na anaanza upya kama mwanachama mpya na anaanza kwa kadi mpya, ndiyo maana amekabidhiwa kadi mpya.

“Niwaombe vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkisema Lowassa asisamehewe kurudi CCM, mnatuambia na nyinyi wa CCM wenye makando kando msisamehewe maana na nyinyi mpo kibao tu na mnavumiliwa. Kila mwanasiasa ana upungufu wake, nasi tunasema mzee Lowassa chama chetu kimekusamehe na tunaungana na chama, tumesahau yaliyopita tunakukaribisha ndani ya chama,” alisema.

Kheri pia alifungua milango kwa kila mmoja kujiunga na CCM bila ya kuulizwa jambo lolote.

“Chama Cha Mapinduzi ni chama cha siasa ambacho kimefungua milango kwa kila raia wa nchi hii kuwa mwanachama. Lowassa ni raia wa nchi, kurudi CCM hakumnyimi haki yake kama leo ambavyo kiongozi yeyote ataamua kujiunga nacho.

“Lowassa aliondoka CCM, ametamani kurudi CCM, sisi kama wanachama tunahitaji kuwa na wanachama wengi, hakuna chama kisichotaka wanachama.

“Lowassa atakuwa mwanachama wa milioni tisa na moja ya kazi ya chama cha siasa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama,” alisema.

UTARATIBU WAFUATWA

Kheri alisema kuwa wamefurahishwa jinsi taratibu zilivyofuatwa wakati Lowassa akirudi ndani ya CCM.

“Lowassa amekwenda kutamka anarudi nyumbani kwanini amesema anarudi nyumbani, anajua mara baada ya kutangaza kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa.

“Ndiyo maana kauli yake ya mwanzo kwamba amerudi nyumbani sio kwamba amerudi CCM, kwa sababu kuna taratibu za kurudi ndani ya chama, ameandika barua kwenye tawi lake akiomba ridhaa ya kuwa mwanachama.

“Tawi lake limejadili kama anavyojadiliwa mwanachama mwingine, wilaya (Monduli) ndiyo imepitisha jina lake, Mungu mbariki mlezi wa chama Mkoa wa Arusha, Humphrey Polepole, ameshiriki katika kikao cha kumpokea Lowassa na hata katika kikao cha mwisho,” alisema.

WAMPA USHAURI

Kheri alimshauri Lowassa kufuata kanuni na taratibu za chama kwa kutambua kwamba kilianzishwa na Mwalimu Julius Nyerere.

“Tunamkaribisha CCM, lazima ajue kwamba chama hiki ndicho kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere na ambacho kilimlea mpaka akaona anastahili kuwa Rais, chama ambacho kilishiriki katika vikao kwamba yeye hatoshi asubiri kwanza, chama hicho ndio kimempokea na kuwa mwanachama wake.

“Hakuna tulichobadilisha katika chama chetu, ni kile kile kilichokuwa mwanzo ndio ambacho kinaendelea,” alisema.

WAKARIBISHA WENGINE

Aidha Kheri aliwataka wanachama wa vyama vingine kumuiga Lowassa kurudi CCM.

“Tumkaribishe Lowassa na sisi tunasema karibu ndugu Lowassa ndani ya chama, lakini tunawaomba uamuzi wa Lowassa uchochee wao kurudi, tunawakaribisha, chama hiki ni cha Watanzania wote,” alisema.

UTEKWAJI WATU

Katika hatua nyingine, Kheri alishangazwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia jina la Usalama wa Taifa na kudai wametekwa.

Alisema lengo la watu hao ni kutaka kuvichafua vyombo vya usalama mbele ya jumuiya na taasisi za kimataifa ili nchi ionekane haifai jambo ambalo si sahihi.

“Nchi yetu ni salama sana, tangu tumeanza mwaka huu hakuna ambaye amesema hakuna usalama katika nchi yetu. Imetokea mtu sasa hivi hata kama alikuwa anadaiwa deni na mdeni wake huko, wakimvizia kumdai deni anasema alitaka kutekwa na Usalama wa Taifa, lipa deni la watu acha kusingizia taasisi za usalama uongo,” alisema Kheri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles