24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uhusiano Tanzania na Kenya ni wa kihistoria

HILAL K SUED

UHUSIANO baina ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria na kama ilivyo ada katika masuala ya historia kuhusu nchi zinazopakana, hakukosi misuguano ya mara kwa mara na ya hapa na pale.

Labda nitaje tu kwamba historia inatuambia kwamba Kenya iliwahi kuivamia nchi yetu hii kijeshi na kuikalia kwa takriban miaka minne hivi. Hiyo ilitokea wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia miaka 100 iliyopita wakati nchi zote hizi mbili zilikuwa zinatawaliwa na wakoloni tofauti – Kenya ikitawaliwa na Waingereza na nchi yetu ikitawaliwa na Wajerumani, wakati huo ikiitwa Deutsch Osta-Afrika (German East Africa).

Mwaka 1914 majeshi ya Waingereza kutoka koloni lao la Kenya yaliingia nchini kupitia maeneo ya kaskazini na kupambana na majeshi ya Ujerumani kwa zaidi ya miaka minne na kuyakimbiza hadi Msumbiji nchi iliyokuwa koloni la Wareno na hatimaye hadi Rhodesia (koloni jingine la Uingereza) ambako ndiko kulisainiwa mkataba wa Wajerumani kusalimu amri – Novemba 1918.

Baada ya miaka minne jumuiya ya Kimataifa (League of Nations) – mtangulizi wa Umoja wa Mataifa – waliikabidhi rasmi nchi hii kwa Waingereza kuitawala chini ya udhamini wa Jumuiya hiyo hadi 1961 tulipopata uhuru wetu.

Lakini hiyo historia ya matukio ya zamani inatuambia chini ya ukoloni wa Uingereza nchi hizi za Afrika ya Mashahriki (Tangayika, Kenya na Uganda) zilikuwa na mahusiano makubwa, hasa ya kiserikali na ushirikiano mzuri na wa karibu zaidi kuliko hata katika kipindi cha baada ya uhuru.

Kwa mfano ushirikiano katika masuala ya forodha baina ya Kenya na Uganda ulianza mwaka 1917 na Tanganyika ilijiunga mwaka 1927. Baada ya hapo mwaka 1948 kuliundwa Tume Kuu ya Afrika Mashariki (East African High Commission –EAHC) iliyowawezesha wakoloni kuzitawala nchi hizi kwa ufanisi zaidi na ushirikiano kwani waliona kwamba wananchi wa nchi hizi walikuwa na mahusiano ya kindugu pia.

EAHC ilidumu hadi 1961 ilipoanzishwa chombo kingine cha ushirikiano – East African Common Services Organization (EACSO) baina ya taasisi mbalimbali za kutoa huduma za kipamoja kama vile huduma ya usafiri wa reli na ule wa ndege, posta na simu na bandari.

EACSO ilienda hadi 1967 ndipo nchi tatu hizi zenyewe zikaanzisha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (East African Community –EAC) ambayo ilidumu miaka kumi tu na kuvunjika kutokana na tofauti zilizojitokeza.

Baadhi ya tofauti hizo zilitokana na madai ya Kenya kutaka vita zaidi katika vyombo vya kutoa maamuzi, kutoelewana na dikteta Idi Amin wa Uganda ambaye alikuwa na mzozo wa kisiasa na Tanzania kutokana na madai kwamba Tanzania ilikuwa inahifadhi vikosi vya kumng’oa madarakani – suala ambalo alisema halikubaliki katika mkataba uliounda jumuiya hiyo.

Aidha kulikuwa na suala la kiitikadi baina ya Tanzania na Kenya kuhusu sera za kiuchumi ambapo Tanzania ilifuata sera za kisoshalisti na Kenya za kibepari.

Pia itakumbukwa kwamba katika kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 1978, Kenya ilionekana kama ilisuka mpango wa jumuiya kuvunjika ambapo iliishia kuhodhi mali nyingi za iliyokuwa EAC, kiasi kwamba wakati wa kuifufua upya ilibidi serikali ya Kenya izilipe fidia Tanzania na Uganda kutokana na kitendo walichofanya mwaka 1978.

Viongozi wa Kenya walionekana hawaitaki Jumuiya na baadhi yao walionekana kusherekea ilipovunjika. Mmoja wa washerehekeaji ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Charles Njonjo.

EAC ya awali ilikuwa na mfumo wa kipekee duniani, uliweka ushirikiano wa karibu zaidi kuliko hata ile Jumuiya ya Ulaya (EU). EAC iliendesha kipamoja huduma za jamii zilizotajwa hapo juu pamoja na Mahakama ya Rufaa, benki ya pamoja ya maendeleo (E. A. Development Bank) taasisi za utafiti wa masuala ya malaria, kilimo, madawa ya kuua wadudu, na mengineyo mengi.

Kusema kweli kuvunjika kwa jumuiya hiyo ilikuwa ni hatua isiyoweza kusameheka kwani nchi tatu hizi zilikuwa zimepoteza miaka 60 ya ushirikiano na faida zake za kiuchumi na masoko.

Hata hivyo EAC ilifufuliwa mwaka 1999 baada ya kutiwa saini mkataba wa kuanzishwa tena lakini haikuwa katika mfumo na ubora wa ile ya awali.

Kwa ujumla tangu kuvunjika kwa EAC ile ya awali lakini hata hivyo mahusiano baina ya Kenya na Tanzania hayakuwahi kuwa manyofu sana na kwa kiwango kikubwa, kwa namna moja au nyingine, mahusiano hayo yamekuwa ya kuvumiliana zaidi kuliko ya urafiki.

Kwa mfano wakati wa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, Tanzania haikufurahia kitendo cha Kenya kufanya biashara na serikali ya Makaburu wa Afrika ya Kusini wakati nchi nyingi ziliamua kuisusia.

Kingine kilichokuwa kinalalamikiwa, hasa kwa Tanzania na Uganda ni tofauti kubwa ya kimaendeleo baina ya Kenya na nchi hizo mbili. Hivyo ilisisitizwa mkataba ulioianzisha EAC ubebe vipengele vya kupendelea Tanzania na Uganda zaidi katika masuala ya uchumi.

Kwa mfano viongozi walitambua tofauti kubwa zilizokuwapo za kimaendeleo hasa maendeleo ya viwanda baina ya Kenya na Tanzania kwani Kenya ilikuwa na viwanda vingi kuliko Tanzania ambayo iligeuzwa kuwa kama ni soko la bidhaa zake.

Hivyo ikaamuliwa kwamba katika kuanzisha viwanda Tanzania na Uganda zipewe kipaumbele. Na ndivyo ilivyokuwa – Tanzania ikapewa kuanzishwa viwanda vya kutengeneza radio (National na Philips) na matairi ya magari (General Tyre).

Baada ya kuvunjika kwa EAC ya awali kulikuwapo kipindi cha misuguano mikubwa baina ya Kenya na Tanzania. Kenya ilikataa usafiri wa reli na ndege kwani wao (Kenya) ndiyo walihodhi injini nyingi za treni za lililokuwa Shirika la Reli la Afrika Mashariki (East African Railways Corporation -EARC) na ndege nyingi za lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (East African Airways –EAA). Makao makuu ya mashirika yote hayo mawili yalikuwa Nairobi.

Aidha katika usafiri wa majini katika Ziwa Victoria meli kubwa pekee MV Victoria nayo ilizuiliwa katika bandari ya Kisumu, Kenya na hivyo kuinyima Tanzania huduma za usafiri.

Eneo kubwa la ziwa hilo liko upande wa Tanzania ambayo ina bandari tatu – Musoma, Mwanza na Bukoba, wakati Kenya ina bandari moja tu – Kisumu.

Aidha kulianza fukuza fukuza ya watanzania waliokuwa wakiishi au kufanya kazi Kenya, kuna baadhi walikuwa wanatolewa majumbani mwao usiku na kupakiwa katika vyombo vya usafiri kurejeshwa Tanzania.

Mawaka 1978 Tanzania ikaanzisha vita na Uganda katika azma ya kumuondoa madarakani Dikteta Idi Amin. Wengi waliona kwamba haikukaa vizuri kwa Tanzania kuanzisha vita na Uganda wakati bado tulikuwa na uhusiano mbaya na Kenya kwani nchi hizo mbili (Uganda na Kenya) zingeweza kushirikiana dhidi ya Tanzania.

Hata hivyo bado haijafahamika iwapo Kenya ilimpa Idi Amin msaada wowote wa hali na mali katika vita yake dhidi ya nchi yetu.

Uhusiano ulioonekana wa kawaida baina ya Kenya na Tanzania ulianza kuonekana kuanzia 1983. Wakati huo mambo mengi yalikuwa yamebadilika – kama vile sera ya Tanzania ya ujamaa ilianza kutoweka na baada ya mgawanyo wa mali na madeni ya iliyokuwa EAC ya zamani.

Lakini hata hivyo uhusiano bado unaendelea kuwa wa kuvumiliana zaodi kuliko urafiki. Kumekuwapo na sintofahamu kuhusu suala la utalii kwani kila nchi ingependa watalii wa nje waingie kwake kwanza ndipo baadaye wasafiri kwa barabara hadi nchi nyingine.

Suala la Tanzania kuingia mkataba na Uganda wa kupitisha mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga halikuifurahisha Kenya kwani wao waliutaka mradi huo hasa kutokana na ukaribu hadi kufikia bandari ya Mombasa.

Mwaka jana kuliibuka suala la kuchomwa vifaranga vya kuku vilivyoagizwa kutoka Kenya na kupigwa mnada wa mamia ya ng’ombe za Kenya zilizoingia nchini kutafuta malisho.  

Kwa upande wao Wakenya wanaona Tanzania haina urafiki mzuri na serikali ya Kenya iliyopo madarakani ya Jubilee, na kwamba Tanzania ina urafiki zaidi na muungano unaoongozwa na Raila Odinga. Hivyo suala la Tanzania kupewa mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda limekuwa ni kichocheo kingine kikubwa cha kuwafanya Wakenya kuwa na hisia hasi kwa Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles