24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sudan na zama mpya zinazofuta ndoto za ‘wajeshi’ kufia madarakani

JOSEPH HIZZA

SASA ni historia, utawala wa Rais Omar al-Bashir umeng’olewa rasmi na Jeshi aliloliamini kwa miaka mingi kumlinda katika namna ambayo iwapo ingetokea miaka angalau mitano iliyopita ingekuwa ngumu kuamini.

Lakini safari hii lilionekana likija na bahati mbaya au nzuri liliharakishwa na ondoko la staili kama hiyo iliyomkumba Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika (82), aliyeng’olewa wiki mbili kabla ya Bashir (75).

Kutabiriwa huko si kulitokana na nguvu mpya waliyopata waandamanaji wa Sudan baada ya wenzao wa Algeria kufanikiwa, bali pia mwenendo mpya unaojionesha mwongo huu kwa tawala za kijeshi kuacha ‘kuwasapoti’ watu wao hasa wale waliokaa madarakani muda mrefu na wenye umri mkubwa.

Watasapoti vipi mtu, ambaye kwa sasa hana mvuto si tu kwa wananchi bali pia jeshi?

Mtu ambaye si tu yu mzee bali pia aliyepoteza nguvu za kiafya, kiakili, kimwili na kiushawishi kwao ni wa kumtupilia mbali.

Majenerali wa Jeshi huwaondoa wanasiasa wanajeshi wao hao waliochoka, ambao licha ya kwamba uwapo wao uliwanufaisha, wanaona bila kufanya hivyo, nao wanaweza kupoteza iwapo nchi itatumbukia katika machafuko.

Hivyo bora inakuwa ni kukiondoa kirusi kimoja au ikibidi pamoja na waliokizunguka, ili wao (majenerali) waendelee kuwapo kufaidi matunda ya nchi.

Kwa sasa kinachotazamwa ni iwapo Sudan itageuka kuwa Misri nyingine, ambayo jeshi ndilo linaloonekana kutawala na kuweka watu wake mwelekeo ambao pia ulishuhudiwa pia nchini Zimbabwe wakati jeshi lilipomng’oa mtu wake Robert Mugabe (95) miezi 17 iliyopita.

Kwa sasa Mugabe amelazwa akitibiwa nchini Singapore.

Hata hivyo, Sudan inaweza isichukue mwelekeo wa Misri, kutokana na waandamanaji wa Sudan kuzidi kuchachamaa tofauti na kwa jirani zao hao, ambako waliliachia jeshi liendelee na mchakato mwingine baada ya kuwafurahisha walipomwondoa mtawala mkongwe Hosni Mubarak (90) mwaka 2011.

Ni wazi jeshi la Sudan halitakuwa tayari kuchafua sifa ililojijengea miongoni mwa umma wa Wasudan wakati iliposikiliza kilio chao kuanzia kuwalinda dhidi ya vyombo vingine vya usalama hadi kuwaondolea mtu wao aliyekataliwa.

Ni kwa vile licha ya kuwafurahisha raia, utawala huo unakabiliwa na shinikizo kubwa si tu kutoka kwa waandamanaji bali pia mataifa ya magharibi kuutaka ukabidhi mamlaka kwa raia.

Mwenendo huo mpya unatokana na jeshi kuunda Baraza la Kijeshi la mpito kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuitisha uchaguzi.

Hatua hiyo, ilitangazwa na Waziri wa Ulinzi, Jenerali Awad Ibn Auf, ambaye pia mbali ya kutangaza hatua mbalimbali ikiwamo kukamatwa kwa Bashir na waliomzunguka alijitangazia kuwa Rais wa Baraza hilo.

Lakini wandamanji waliapa kubakia mitaani hata baada ya hatua hiyo, wakitaka mageuzi na kuidhinishwa kwa serikali ya kiraia mara moja.

Kuona mambo ni magumu, Ibn Auf alitangaza kujiuzuliu siku ya pili, kama alivyojiuzulu mkuu wa usalama anayeogopwa na wengi Jenerali Salah Gosh.

Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan akatajwa kuwa kiongozi wa baraza hilo.

Lakini waandamanaji bado wapo katika makao makuu ya jeshi kwa siku ya 12 sasa tangu walipohamishia hapo kuomba msaada wa jeshi baada ya kushuhudia mafanikio ya Algeria.

Safari hii wanataka utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo hali ambayo imelilazimisha jeshi kuwataka wapinzani wachague mtu wa kushika wadhifa wa waziri mkuu.

Licha ya ugumu wa kubashiri uwezekano wa jeshi kuhodhi madaraka kama ilivyo Misri, Sudan pamoja na Algeria, ambako jeshi pia limehodhi madaraka zinaweza kirahisi kukumbushia kilichotokea katika mapinduzi ya Misri na Tunisia mwaka 2010 na 2011.

Kama majirani zao, waandamanaji wa Sudan na Algeria waliweza kuziangusha tawala za kiimla za miongo kadhaa kwa kipindi cha miezi michache tu na bila kutumia bunduki.

Maandamano, kupaza sauti, kupinga na udhubutu wa watu wa Sudan na Algeria ikishadidiwa na miito yao ya kutaka uhuru na demokrasia hadi walipoweza kuwashawishi na kuwasalimisha amri wanajeshi.

Lakini pia mapinduzi ya Sudan na Algeria ni kama yale ya Tunisia na Misri, ambako yalikuwa mbali na machafuko na kudhihitrisha nguvu ya maandamano ya amani. 

Ukiachana na hayo, turudie katika mada yetu kuwa kung’olewa kwa mtawala mwingine mkongwe barani Afrika kumetoa funzo wa watawala wa aina hiyo kuwa kadiri wanapozeeka na nguvu zao kupungua ndipo uwezekano mkubwa wa kutoswa mithili ya tambala bovu unapokuja.

Kama tulivyoona hapo juu, katika kipindi cha muongo huu unaoelekea ukingoni yametokea nchini Misri, Zimbabwe, Algeria na sasa Sudan huku Gambia ikiwa ni mfano mdogo tu.

Kote kuna mfanano wa mambo kuanzia namna walivyoingia madarakani, wakitokea jeshini na kutawala kwa miaka mingi wakiwa katika hali ya uzee na hata ugonjwa.

Gambia ni tofauti kidogo, Yahya Jammeh aliyeingia kwa mapinduzi alitawala kwa miaka 23 hadi alipong’olewa mwaka 2017 wakati aliposhindwa uchaguzi huku jeshi likikaa pembeni bila kumsaidia angalau umri wake si mkubwa hadi leo akiwa nje ya madaraka hajafikisha miaka 60.

Pengine ni kutokana na kuingia madarakani katika umri wa ujana wa 29 akatawala kwa zaidi ya miongo miwili na kutoswa akiwa bado katika hali ya ‘ujana.’

Mataifa hayo mengine, umri wa viongozi wao Ben Ali wa Tunisia, Mubarak, Mugabe, Bouteflika na Bashir wakati waking’olewa ulianzia miaka zaidi ya 70 hadi zaidi ya 90.

Mifano ya yaliyotokea katika mataifa, ambayo jeshi limehodhi siasa na uchumi kama vile Misri na Zimbabwe inaweza kuakisi taswira ya baadaye ya watawala wa aina hiyo waliobakia barani Afrika.

Tukianzia mfano wa Misri, Jenerali Mubarak aliyetawala kwa miaka 30, akiingia mapema miaka ya 1980 baada ya kuuawa kwa mwanajeshi mwingine Nasser Sadat.

Mwaka 2011 kufuatia maandamano makubwa ya miezi kadhaa ambayo hayakuwahi kuonekana katika taifa lililoongozwa kijeshi na mkono wa chuma, Jeshi la Misri lilijitosa na kuuruhusu umma kumpindua Rais Mubarak katika mazingira ambayo yalisifiwa sana si tu nchini humo bali pia jumuiya ya kimataifa.

Walio wengi hawakujua kuwa Jeshi lilikuwa limemchoka Mubaraka, likichukizwa na harakati zake za kutaka kuwarithisha urais watoto wake, wakiwahesabu tishio kwa masilahi yao jeshini.

Hivyo, basi ili kuwafurahisha Wamisri japo kwa muda jeshi likamruhusu Mohamed Morsi kuchukua urais na kuunda serikali baada ya kushinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia usio na chembe ya jeshi.

Lakini lilimruhusu atawale kwa mwaka mmoja tu kisha likatafuta visingizio vya hapa na pale kutafuta uhalali wa kumwondoa na kufunga milango na juhudi zozote za kundi la kisiasa la rais huyo, Muslim Brotherhood kisha kumpindua.

Kwa vile Morsi hakuwa chaguo la jeshi bali wananchi, hivyo basi haikuwa ajabu kutodumu kwani aling’olewa na Mkuu wa Majeshi, Abdel Fattah el-Sisi ambaye ndiye rais hadi sasa. 

Kwa maana hiyo, Jeshi la Misri limewachagulia Wamisri viongozi tangu zama za kina Gamal Abdel Nasser, Sadat Anwar, Hosni Mubarak na sasa el-Sisi, wote wakitokea jeshini.

Ni hali ambayo imeonekana katika taifa la Zimbabwe. Ikipata uhuru wake mwaka 1980, Zimbabwe iliongozwa na Rais Canaan Banana, lakini mamlaka yalionekana zaidi mikononi mwa Mugabe aliyekuwa waziri Mkuu akitokea jeshini.

Kwa msaada wa jeshi, Mugabe akaja kuitawala  Zimbabwe kwa zaidi ya miaka 30 hadi Novemba mwaka juzi. 

Akiwa na umri wa miaka 94, alipinduliwa na jeshi alilolichukiza kwa kitendo chake cha kuruhusu kizazi cha vijana wadogo wasiojua harakati za uhuru wa Zimbabwe wakiongozwa na mkewe Grace Mugabe kuiendesha nchi watakavyo.

Likiona namna maslahi yake yanavyojaribiwa, Jeshi likiongozwa na Jenerali Costantino Chiwenga likampindua Mugabe Novemba mwaka jana na kumweka mtu wao Emmerson Mnangagwa.

Chiwenga akateuliwa na Mnangagwa kuwa makamu wa rais.

Ikafuatia Algeria, Bouteflika ni mjeshi aliyeletwa na jeshi kutuliza dhidi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 2000. Akatawala kwa miaka 20, lakini karibu nusu ya muda huo akiwa mgonjwa asiyeweza kuzungumza wala kuendesha kampeni lakini kivuli chake kikawa kikishinda chaguzi.

Lakini wananchi safari hii hawakukubali hilo, wakaandamana tangu mwaka jana na kulifanya jeshi kuamua kumweka pembeni. 

Nguvu zilizotumika na matumizi ya jeshi badala ya askari polisi tu zimeashiria namna watawala wa kijeshi wasivyo tayari kuachia madaraka kirahisi kwa tawala za kiraia wanazohisi zitaondoa masilahi waliyofurahia kwa miaka mingi.

Hilo linamaanisha kung’olewa kwa watawala hao si tu kumetokana na kuchokwa hata na watu wao (wanajeshi) bali pia wenyewe kuchoka kimwili na kiakili na hivyo kukosa nguvu zile za awali zilizowawezesha kulidhibiti jeshi na nchi.

Ni fikra potofu kwa watawala wa aina hii kudhani kwamba kwa unono na uhuru mkubwa wanaoliachia jeshi basi watalindwa milele madarakani hata pale watakapochoka.

Watawala wa aina hii wanatakiwa kusoma alama za nyakati kuondoka mapema kwa heshima kabla ya fedheha haijawakumba katika uzee wao na kuwakosesha amani kipindi kifupi cha maisha kilichobaki hapa duniani.

Katika hali ambazo nchi majeshi hutawala kupitia watu wao, wakati zinaposimama kwa ukubwa wa maandamano, ambayo si rahisi kuyazuia bila damu nyingi kumwagika, majeshi huwa hayana namna nyingine nzuri.

Zaidi ya kuwafutilia mbali watu wao, ambao kwao hawana kazi tena wala nguvu za udhibiti, ambao kwa wakati huo huwa mikononi mwao.

Baada ya kuviondoa ‘virusi’ hivi huku wakijifanya wako upande wa raia, majeshi ‘hu-test mitambo’ ya waandamanaji wakija na hatua hatua mbalimbali, ambazo ukiziangalia utaona zinalenga kutafuta mtu wanayemkubali akalie Ikulu kuendeleza maslahi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles