31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Simba SC wakiyafanya haya, robo fainali inawahusu

BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

‘DO or DIE’ ni ujumbe ambao utatumika leo kwa kila timu kuelekea michezo ya mwisho ya Klabu Bingwa Afrika hatua ya 16 bora.

Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam patakuwa hapatoshi, huku Simba SC wakishuka dimbani na kuwakaribisha wapinzani wao, AS Vita Club kutoka nchini Kongo.

Hakuna anayehitaji sare kwenye michezo hiyo, hivyo lazima tushuhudie ushindani wa hali ya juu kuanzia nje hadi ndani ya uwanja.

Leo Simba watakuwa uwanjani, huku wakiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 5-0, walichokipata katika mchezo wa awali dhidi ya wapinzani hao nchini Kongo.

Kuelekea mchezo wa Simba, wachambuzi mbalimbali wameuelezea mchezo huo juu ya vitu gani vifanyike ili kuweza kuipeperusha vema bendera ya timu hiyo.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo Simba SC wakiweza kuyaweka sawa, basi AS Vita Club hawawezi kutoka kwenye uwanja wa Taifa leo.

Ulinzi

Simba SC wanatakiwa kuhakikisha wanaweka ulinzi wa kutosha kwa wapinzani wao katika kipindi chote cha dakika 90, hata kama mpinzani hana mpira.

Kwa kufanya hivyo, wataweza kuwanyima nafasi wapinzani hao kutengeneza mipira ya hatari kama walivyofanya mchezo wao wa awali.

Ulinzi kila idara ukiwa imara wataweza kupunguza kasi ya wapinzani wao, kikubwa kwa Simba si kulipa kipigo cha mabao matano, ila cha kukiangalia ni ushindi wa aina yoyote, kikubwa ni pointi tatu ambazo zitawafanya wavuke na kuingia hatua ya robo fainali.

Uwepo wa Erasto Nyoni ndani ya kikosi cha Simba unaweza kuongeza uimara katika safu hiyo ya ulinzi kutokana na uzoefu wake, japokuwa amekuwa nje ya uwanja kwa muda.

Beki wa kati, Pascal Wawa, anatakiwa kuwa makini kwa kuweka ukuta wake sawa sawa, mchezaji huyo amekuwa akijiamini sana na kumfanya wakati mwingine asogee mbele kwa ajili ya kwenda kushambulia, kitu ambacho kinaweza kuigharimu timu.

Wasibweteke uwanja kujaa

Siku zote shabiki anadaiwa kuwa mchezaji wa 12, lakini hiyo inatokana na idadi kubwa ya mashabiki ambao watajitokeza kuwasapoti wachezaji wao.

Ni wazi kwamba, kuna asilimia kubwa ya mashabiki wa Simba SC kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuipa nguvu timu yao, tofauti na wale wa AS Vita, ambao watafunga safari kutoka nchini Kongo.

Nguvu kutoka kwa mashabiki waliojitokeza inawafanya wachezaji kuwa na furaha na kujiamini, lakini hilo si la kulitegemea sana, kujaa kwa mashabiki wa Simba uwanjani kusiwe tegemeo sana, kikubwa ambacho wachezaji wanatakiwa kukiangalia ni kuhakikisha wanaipigania timu na mashabiki hao waliojitokeza.

Kumiliki mpira

Timu yoyote ambayo ina uwezo mkubwa wa kumiliki mchezo inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri ndani ya dakika 90 kwa kuweza kupata matokeo.

Hivyo Simba wanatakiwa kuhakikisha wanaweza kumiliki mchezo huo kwa kipindi chote, hasa katika safu ya kiungo ambayo AS Vita wanaitegemea kwa kuanzisha mashambulizi yao.

Sina wasiwasi sana na ubora wa safu ya kiungo ya Simba, lakini kumkosa kiungo imara wa timu hiyo, Jonas Mkude kutokana na kutumikia kadi za njano kunaweza kukaifanya safu hiyo ikapwaya.

Lakini kwa kuwa Simba ina wachezaji wengi wenye kucheza nafasi hiyo, ninaamini Kocha Mkuu, Patrick Aussems na benchi lake la ufundi wameliona hilo na wamejipanga kwa kulifanyia kazi, hivyo wataweza kuliziba pengo hilo.

Kazi kubwa ya viungo iwe ni kupunguza makali ya wapinzani pamoja na kuweza kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji, huku wachezaji kama Clatous Chama awe na jukumu la kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji na akipata nafasi anyooshe msuli kwa kujaribu kupiga mashuti ya mbali ya kulenga lango.

Mipira ya kona

Mchezo wa awali ambao Simba waliupoteza kwa mabao matano, baadhi ya mabao hayo yalitokana na mipira ya kona ambapo walinzi wa Simba walionekana kukosa umakini wa mipira hiyo.

Wachezaji wa AS Vita Club ni wazuri kwa mipira hiyo na ile ya adhabu katika eneo la hatari, hivyo Simba wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa makini na matukio hayo kwa kuwakaba wapinzani kila sekunde, kwa kuwa ni warefu, hivyo wasipate nafasi ya kufanya maandalizi wakiwa kwenye eneo la hatari.

Ninaamini kocha huyo wa Simba, Patrick Aussems, aliyaona makosa ambayo waliyafanya wachezaji wake kwenye mchezo ule wa Kongo na kuyafanyia kazi makosa waliyoyafanya.

Mlinda mlango

Kipa namba moja wa Simba SC, Aishi Manula, awe mstari wa mbele kuhakikisha anawapanga wachezaji wake kila wakati ili waweze kuwa bora kwa kuwazuia wapinzani wasiwe na madhara.

Kipa ni mchezaji wa pekee ambaye anaweza kuutazama mchezo wote na kuwaangalia wachezaji jinsi walivyojipanga, hivyo awe anajitahidi kuwakumbusha wachezaji wake pale wanapojisahau kutekeleza majukumu yao.

Kila mchezaji anapaswa kutekeleza majukumu yake, lakini kuna wakati anashindwa kufanya hivyo kutokana na kuchanganyikiwa na ukubwa wa mchezo wenyewe.

Washambuliaji

Hakuna shaka katika ubora wa washambuliaji wa Simba, Medie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi, wamekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu pale wanapopata nafasi ya kuwa pamoja katika safu ya ushambuliaji.

Kasi yao imekuwa ikifanya vizuri siku hadi siku, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla wanaifanya wikiendi hii kuwa ya furaha kwao endapo wataweza kuipeleka timu hiyo katika hatua ya robo fainali.

Kufa au kupona kunaweza kuwafanya Simba SC wakautumia vizuri uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki zao.

Huu ni mchezo ambao unaweza kutengeneza historia mpya kabisa kwa baadhi ya wachezaji wa Simba endapo wataipeleka robo fainali.

Bocco, Manula, Nyoni, Mohammed Hussein, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na wengine watakuwa na kitu cha kuja kusimulia kwa wajukuu hapo baadaye endapo wataipeleka timu robo fainali ya Barani Afrika.

Miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya soka ndani ya nje ya nchi, Robert Ajwang’, anaamini Simba wana nafasi kubwa ya kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani leo na kuwapa furaha mashabiki endapo kila mchezaji ataamua kujitoa kwa kufa au kupona na kutimiza majukumu yao.

Kila la heri Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kwa ajili ya faida ya soka la nchi. Hakuna kinachoshindikana (Do or Die Try).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles