33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Prof:Lipumba ateua wakurugenzi CUF

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameteua wakurugenzi wa nafasi mbalimbali pamoja na viongozi wa jumuiya za chama hicho.

Profesa Lipumba amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ibara ya 91 (1) (f), ambayo inamtaka kuteua kutoka miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na wanachama jasiri.

Wanachama walioteuliwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Zainab Mndolwa na naibu wake, Omar Mohammed Omar, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera, Mohammed Habibu Mnyaa na naibu wake, Mohammed Ngulangwa.

Wengine ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar na naibu wake, Mohammed Vuai Makame, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya na naibu wake, Mbarouk Seif Salim.

Wengine ni Haroub Mohammed Shamis aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, naibu wake Salvatory Magafu wakati Thinney Juma Mohammed akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mafunzo na Uhamasishaji na naibu wake, Masoud Omary Mhina.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema Kamati ya Uongozi imemteua Yusuph Mohammed Mbugiro kuwa Ofisa Tawala wa ofisi kuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti huyo wa CUF pia amefanya uteuzi wa viongozi wa jumuiya za chama huku akisema viongozi hao watakaimu nafasi zao mpaka pale watakapochaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

“Kwa kuzingatia hali ya jumuiya zilivyo sasa, nateua makaimu wenyeviti na makamu wenyeviti na makaimu katibu watendaji na manaibu wao katika jumuiya zote za chama watakaoratibu na kukamilisha uchaguzi wa jumuiya za chama,”alisema Lipumba.

Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali ameteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), makamu wake Faki Suleiman Khatib na kaimu Katibu Mtendaji, Yusuph Kaiza Makame na naibu wake, Mbaraka Chilumba.

Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (Jukecuf) ni Dhifaa Mohammed Bakar na makamu wake ni Kiza Mayeye, kaimu Katibu Mtendaji ni Anna Ryoba na naibu wake ni Leila Jabir Haji.

Kwa upande wa Jumuiya ya Wazee wa Cuf (Juzecuf), kaimu mwenyekiti ni Mzee Chunga na makamu wake ni Hamida Abdallah, kaimu katibu mtendaji ni Hamis Makapa na naibu wake ni Said Ali Salim.

Profesa Lipumba amefanya uteuzi huo baada ya CUF kupitia kipindi kirefu cha mgogoro ulioibua makundi mawili ya CUF Lipumba na jingine likiwa chini ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mgogoro huo ulianza baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti Agosti mwaka 2015 baada ya kutokubaliana na uamuzi wa vyama washirika wa Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa kugombea urais.

Lakini mwaka mmoja baadaye alitengua barua yake ya kujiuzulu na kutaka kurejea kwenye nafasi yake, jambo lililosababisha mgogoro hadi Maalim Seif na wafuasi wake walipoamua kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles