29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Njia sahihi ya kulipa kisasi ni kumwonyesha upendo aliyekuudhi

CHRISTIAN BWAYA

NILIWAHI kupishana na mtu ambaye awali tulikuwa karibu kikazi.  Tulifahamiana kwa muda mrefu na nilimwamini kama rafiki tuliyefanya kazi pamoja kufikia malengo ya pamoja.

Sikuwahi kufikiri siku moja angeweza kunihujumu kwa malengo yake binafsi. Kilichoniudhi si tu kukosewa kwa makusudi, bali kuona mtu niliyemheshimu na kumwamini kwa muda mrefu alikuwa anajaribu kufikia malengo yake kwa kuniharibia kazi yangu. Kwa lugha nyingine mafanikio yangu yalitegemea kazi yangu kuharibika. Nilijisikia vibaya.

Uhusiano wetu ulizorota kwa muda. Baadae ilibidi tuzungumze. Alinieleza namna mazingira yalivyochangia yeye kufanya kile alichokifanya. Alijutia makosa na nikaamini nimemsamehe.

Hata hivyo, ninapotazama nyuma hivi leo ninagundua kuwa sikuwahi kumsamehe kwa takribani miaka miwili baadae. Uhusiano wetu uliendelea kuzorota na haukuweza kurudi kama ilivyokuwa hapo kabla. Ingawa tuliendelea kuzungumza lakini ule urafiki unaoanzia moyoni haukuwapo.

Sikuwa na imani naye. Sikuamini aliyoyasema na kuyafanya. Kila nilipokumbuka namna alivyonihujumu, hisia za usaliti zilinirudia. Ingawa nilijiaminisha kwamba nimemsamehe, lakini katika maisha halisi sikuwa nimemsamehe.

Kwanza kabisa, wakati wote akili yangu ilikumbuka yale aliyonitendea. Nilikuwa ‘nimemsamehe’ kwa maneno lakini si kwa vitendo. Mara kadhaa moyo wangu ulijaa huzuni na ghadhabu nilipokumbuka kitendo alichokuwa amekifanya. Nikagundua sikuweza kumsamehe kwa vitendo.

Lakini pili, sikuwa natamani kusikia akipatwa na mema. Kama ningesikia akisifiwa kwa jambo zuri alilolitenda, moyoni nilijisikia vibaya. Mafanikio yake yaliniudhi, sifa zake zilikuwa kero kwangu. Moyoni nilitamani kusikia akipata mshahara wa mabaya aliyonitendea. Wahindi wanaita ‘karma.’

Nakumbuka siku moja alipatwa na changamoto fulani kazini. Niliposikia moyo uliruka ruka kwa furaha licha ya kwamba sikusema. Niliamini ‘mungu’ amemlipa kwa mabaya aliyonitendea. Nilifurahia kwamba hatimaye amekula matunda ya matendo yake mwenyewe. Kimsingi, hiki kilikuwa ni kisasi cha kificho hata kama kwa nje niliamini nimemsamehe.

Hali hii ya kutokusamehe ilipanda ngazi na kugeuka kuwa chuki. Sikutamani kuwa karibu naye tena. Chuki iliyokuwa inanitafuna moyoni ilinifanya nikawa mwepesi kutafuta kusikia mabaya na mapungufu yake. Nilijikabidhi kuwa mtumwa wake.

Unapomchukia mtu, kwa hakika, unajibebesha mzigo mzito kihisia kama ilivyokuwa kwangu. Unakuwa na kazi na kupambana na mtu ambaye pengine hana habari na wewe. Wakati wewe ukijiumiza kwa kutamani aharibikiwe, mwenzako ndio kwanza anafanikiwa. Chuki, katika mazingira haya, inakuwa na kazi ya kukuumiza wewe kuliko inavyomwumiza unayemchukia.

Hatimaye nilijifunza kusamehe. Nikagundua unapomsamehe mtu maana yake si tu unasahau kile alichokufanyia, bali unarejesha uhusiano uliokuwapo kabla ya kosa. Kiashiria kimojawapo kwamba umerejesha uhusiano ni pale unapoanza kufurahia mafanikio yake na kusikitika unaposikia amepatwa na mabaya. Hiki ndicho kipimo cha msamaha wa kweli. Kinyume na hapo ni chuki inayoishi ndani yako.

Inawezekana unaposoma hapa unakumbuka watu waliokukosea. Pengine ni mume wako au mke wako. Pengine ni mwanao. Pengine ni ndugu yako wa karibu, mfanyakazi mwenzako au mshirika wako wa kibiashara. Unapokumbuka aliyokufanyia unahisi uchungu. Unajiapiza hutakaa usamehe. Huo ndio utumwa ambao chuki inaweza kukutengenezea.

Kuushinda utumwa huu ni kuwaruhusu watu kukukosea. Nilipojifunza kujiondoa kwenye hadhi ya kuwa mtu maalumu asiyepaswa kuguswa na mwingine, ilikuwa rahisi kuanza ukurasa mpya. Nilianza kuachana na gereza la ‘karma’ la kufikiri kwa kuwa mtu amenikosea, lazima na yeye apatwe na mabaya.

Unaweza kufanya hivyo pia. Msamehe yeyote aliyekutendea mabaya. Hufanyi hivyo kumsaidia yeye kwa sababu pengine anafurahia kukuona unateseka. Unasamehe kwa faida yako mwenyewe. Badala ya kujifungia kwenye gereza la kulipiza kisasi, unajiwekea mazingira ya kuushinda ubaya kwa wema.

Ikiwa ni lazima kulipiza kisasi ili ujisikie ahueni moyoni mwako, kisasi sahihi zaidi ni upendo. Mpende mchumba aliyekuacha, mpende rafiki aliyekusaliti. Mpende mfanyakazi aliyekuhujumu, kwa kufanya hivyo, unajiweka huru wewe mwenyewe na kujifungulia milango ya kusonga mbele na maisha.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles