27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mussa Kilakala: Mwenyekiti UVCCM aliyekuja na ‘Dar ya Kijani’

*Aeleza mkakati kurejesha mitaa, majimbo mikononi mwa CCM

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

HIVI karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa wa vijana kushiriki katika siasa ama kutaka kujua mambo yanayohusiana na siasa.

Tumeshuhudia katika chaguzi za hivi karibuni vijana wamekuwa ndiyo hazina kuu katika siasa wakitumika kutoa hamasa au kuchochea mabadiliko ya kimfumo.

Sote ni mashahidi kwamba, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vijana wametumika kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani mkubwa kwa wanasiasa.

Iliwabidi wagombea kutumia mbinu ambazo zingewavuta kwa wingi vijana, jambo hili halikuwa baya hasa ukizingatia vijana ndio nguvu kazi ya Taifa.

Vijana walifanikiwa kujenga ngome kubwa kwa mgombea huyo, hata wasanii waliokuwa wakitumbuiza katika jukwaa la CCM asilimia kubwa walikuwa vijana.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa uhai wake aliwahi kusema: “Tunataka kuona katika Taifa hili vijana shupavu na wenye kujiamini.

“Si vijana waoga, kina ndiyo bwana mkubwa, vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kijamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania. Tunataka vijana waasi dhidi ya mifumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa,” Mwisho wa kunukuu.

Swali ni Je, vijana wa Tanzania tunaenzi maneno ya Baba wa taifa letu kwa namna gani?

Jibu hilo sasa linawekwa wazi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, ambapo katika mazungumzo yake na MTANZANIA juu ya mikakati kadhaa ya umoja huo kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Alisema kwa kuliona hilo na wajibu wa vijana anaowaongoza katika Mkoa wa Dar es Salaam, walikaa na kuamua kuja na mkakati kabambe ambao utasaidia kurejesha mitaa, kata na majimbo yote kuwa katika mikono ya CCM.

Kilakala alisema kuwa hatua ya UVCCM sasa kuamua kuja na kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’  yenye lengo la kurudisha mitaa na majimbo yaliyokwenda upinzani inakwenda kuifanya CCM kuwa chama imara zaidi na chenye kukubalika mbele ya umma.

Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kampeni hiyo itachochea ustawi zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuzidi kuikita mizizi katika ngazi zote kuanzia mkoa hadi majimbo, wilaya hadi kata, matawi hadi mitaa.

“Tumezindua kampeni yetu ya Dar es Salaam ya Kijani kuelekea serikali za mitaa 2019, kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM mitaa iliyopotea katika uchaguzi uliopita ambayo kwayo itatusaidia kupata ushindi mkubwa kimkoa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa udiwani, ubunge na urais.

“Sote tu mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 wa Serikali za Mitaa na ule Uchaguzi Mkuu wa 2015 tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na majimbo yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM.

“Na sababu za kupoteza huko zinajulikana, sina haja ya kuzirejea sasa. Hivyo sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya chama chetu na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza malengo ya uwepo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola,” alisema Kilakala

Kiongozi huyo wa UVCCM mwenye maono ya mbali ndani ya CCM alisema chama hicho tawala kinahitaji ushindi mkubwa kwa kuweka mikakati ya awali kwa kuwahusisha wanachama wa chama hicho wa ngazi zote.

“Kampeni yetu hii itashuka katika wilaya, kata na matawi yote katika mkoa wetu ili kuwa na ufahamu wa pamoja na kuhakikisha kila kijana wa UVCCM anawajibika ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani yaani Dar es Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati wa uchaguzi tuvune wapiga kura wa kutosha.

KUandaa wapiga kura

Akizungumzia umuhimu wa kampeni hiyo ya Dar ya kijani, Kilakala, alisema kuwa mpango huo utajikita pia kuandaa wapiga kura wajao.

“Kama mjuavyo tutakuwa na maboresho ya Daftari  la Kudumu la Wapiga kura na tunatambua kuwa wapo vijana wenzetu ambao katika uchaguzi uliopita aidha hawakuwa wametimiza umri wa kupiga kura ama walikuwa na vigezo lakini walipuuzia kujiandikisha.

“Tunahitaji kuwatambua vijana hao katika mitaa yetu na taasisi za kielimu, tuwashawishi kujumuika na itikadi ya chama chetu (CCM) na kisha kuwahamasisha wajiandikishe kupiga kura. Kura ni suala la mahesabu na mahesabu kamwe hayaongopi, zinapokuwa nyingi na zilizoandaliwa vyema basi huleta uhakika wa ushindi mkubwa.

“Nani asiyejua kuwa haba na haba hujaza kibaba, tunaamini hili likifanikiwa ipasavyo litachangia kuongeza kura kwa CCM na kufikia malengo tunayoyakusudia ikiwamo kuendelea kushika dola,” alisema Kilakala

Vijana na uongozi

Alisema kuwa anatambua kwamba katika baadhi ya mitaa wapo vijana wengi wanaokubalika na wananchi katika maeneo yao na wanao uwezo mkubwa wa kuongoza.

“Hivyo, tutatumia fursa hiyo kuhakikisha vijana wengi wanajitokeza kugombea na kupiga kura ndani ya chama wakati ukifika ili kuchagiza ushindi wetu.

“Katika miongoni mwa mitaa na kata tulizozipoteza, sababu mojawapo ilikuwa vijana wanaokubalika kutojitokeza kugombea na kuwaachia watu wasiokubalika na hivyo tukashindwa kirahisi na wapinzani wetu. Safari hii hatutafanya kosa hilo, tutatimiza wajibu wetu huu ipasavyo,” alisema

Shukrani kwa Rais Dk. Magufuli

Kilakala alisema anatambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ikiwamo kutatua changamoto za wananchi kwa wakati pamoja na utekelezaji wa kasi wa miradi mikubwa ya maendeleo.

“Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatoa pongezi zangu za dhati kwa niaba ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa na Rais Dk. John Magufuli kwa kutuongoza vyema kupitia Serikali yetu ya CCM katika jukumu la kutatua changamoto za Watanzania na kuwaletea maendeleo.

“Tumejionea dhahiri shahiri namna yale yaliyochelewa yakiwahishwa, yaliyoshindikana yakiwezekana, magumu yakiwa mepesi; yaliyokwama yakikwamuliwa.  Kipekee kwa upande wa vijana tumeendelea kuaminiwa katika Serikali yetu na kupewa majukumu mbalimbali ili nasi tutoe mchango wetu katika kuhuisha hali ya maisha ya watu wetu na ustawi wa nchi kwa ujumla.

“Sisi Vijana wa Dar es Salaam tunamuombea kila jema lenye kheri naye na tunamuahidi kuwa tupo pamoja naye wakati wote!,” alisema Kilakala

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles