23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa kupokea watalii 300 kutoka China

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni  ya Touchroad Group ya China, He Liehui  jijini Dodoma jana.

MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kundi la watalii wasiopungua 300 litawasili nchini Machi.

 Alisema watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili nchini mwaka huu chini ya mpango unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na Kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.

Hayo aliyasema jana ofsini kwake Mlimwa jijini hapa baada ya kukutana na Mwenyekiti wa TouchRoad, Liehui He na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Thomas Mihayo.

Majaliwa alifikia uamuzi wa kuwapokea wageni hao baada ya kuelezwa na He kwamba kundi hilo la watalii 300 likiwa Djibouti litapokewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na likienda Zimbabwe litapokewa na Rais.

 “Tanzania imeamua kuweka mkakati wa kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe za bahari na milima.

“Kwahiyo, ujio wa kundi hili kubwa unatoa fursa mpya ya kutangaza vivutio vya nchi yetu.

 “Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya jirani na vivutio vyetu, wachangamkie fursa ya ujio wa watalii hawa katika maeneo mbalimbali.

“Wakifika Dar es Salaam wanaweza kwenda Kigoma kuona Ziwa Tanganyika, mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini, Arusha au vivutio vya Zanzibar. Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa mbalimbali,” alisema Majaliwa.

Naye Mwenyekiti wa TouchRoad, He alisema kwamba amefurahishwa na wazo lao la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu cha utalii kwa makundi ya watalii ambayo yatakuja Tanzania na baadaye kwenda Lusaka, Harare, Johannesburg na Djibouti.

He ambaye aliwasili nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31 ambao unajumuisha waandishi wa habari, wasanii, wanamuziki na watu mashuhuri.

Akiwa Beijing, China, wakati akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na China Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na uongozi wa TouchRoad ambayo ilionesha nia ya kutangaza fursa za utalii zilizopo hapa nchini.

 Ziara ya He ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya TouchRoad na Bodi ya Utalii ya Tanzania, Novemba mwaka jana.

 Awali He alimweleza Waziri Mkuu nia ya kampuni hiyo kutekeleza makubaliano yao ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko la China ili kuvutia watalii wapatao 10,000 waitembelee Tanzania mwaka huu.

 “Tumepanga kuleta watalii 10,000 kwa mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la kuongeza idadi hiyo kwa asilimia 20 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano. Pia tuna lengo la kuitumia ndege ya ATCL ili ilete watalii moja kwa moja kutoka Shanghai, China,” alisema.

Akielezea ujio wa kundi la kwanza la watalii, He alisema litakaa Djibouti kwa siku moja, Tanzania siku nne na Zimbabwe siku tatu  na kisha kurejea China.

Alisema wanapanga kila mwezi wawe na kundi kubwa la watalii ambao watakuwa wanafikia Tanzania na kupelekwa nchi nyingine kwa sababu Wachina wengi hupenda kufanya utalii kwa siku walau 10, lakini wapelekwe maeneo matatu au manne tofauti kuona vivutio vya aina nyingine badala ya kukaa sehemu moja kwa kipindi chote hicho.

 “Watalii hawa wakija kwa siku tatu au nne wana uhakika wa kutumia Dola za Marekani zaidi ya 2,000, wakienda eneo jingine watatumia fedha pia, namna hiyo tuna uhakika wa kuongeza pato la taifa, lakini pia tuna uhakika wa kutengeneza ajira kwa Watanzania,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles