27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Katakata umeme yaanza

Mwandishi Wetu -Zanzibar

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (Zeco), limesema Shirika la umeme nchini (Tanesco), litaanza kutoa umeme kwa  mgawo Bara na Visiwani kutokana na kufanya matengenezo kwenye eneo la Ubungo.

Hata hivyo, MTANZANIA Jumamosi lilipowasiliana na Tanesco kupitia kwa Kaimu Meneja Mawasiliano, Leila Muhaji, alisema kwa upande wa Tanzania Bara hakutakuwa na mgawo isipokuwa kutakuwa na ukarabati wa mitambo ambao utalazimu kukata umeme kwa baadhi ya nyakati.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Uhusiano wa Zeco, Salum Abdallah Hassan, alisema mgawo huo umeanza jana na kwamba utadumu hadi mwezi Juni mwaka huu.

Alisema mgawo huo utakaochukua miezi minne umeanza jana Februari 22 hadi Juni na utaanza saa 3 asubuhi hadi saa 3.30 usiku na kila eneo litakosa umeme kwa muda wa saa mbili.

“Wananchi watakuwa wanazimiwa umeme na kupata kwa mgawo na hali hiyo itaendelea hadi mwezi wa sita matengenezo yatakapokamilika,” alisema.

Kutokana na hatua hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Zeco, imesema inajipanga kutafuta mbinu mbadala ya kupata umeme wa ziada ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wake pindi umeme mkubwa  wa Tanesco ukikatika kutoka Tanzania Bara.

Salum aliwataka wananchi hususan wafanyabiashara wanaotumia umeme kwa kiwango kikubwa  kuwa wavumilivu kwani shirika hilo wanatengeneza ili kuleta maendeleo nchini.

Alisema Serikali inatambua kuwa umeme ni nishati muhimu kwa wananchi na ndio maana inafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo bila usumbufu.

“Nishati ya umeme imekuwa ni moja ya mambo muhimu katika maisha ya watu lakini sisi tunadhamiria kuimarisha huduma hii ili iwe endelevu na yenye uhakika kwa Wazanzibari,” alisema.

Alisema mgawo huo utawahusisha moja kwa moja wakazi wa Visiwa vya Unguja tu wanaotegemea umeme kutoka Tanzania Bara.

Alisema kwa wakazi wa kisiwa cha Pemba hawataguswa kwa kuwa umeme wanaoutumia ni ule unaozalishwa Tanga.

MAJIBU YA TANESCO

Jana gazeti hili liliwasiliana kwa njia ya simu na Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Muhaji, ili kutaka kufahamu namna upande wa Tanzania Bara utakavyoathirika na matengenezo hayo ambapo alisema hawezi kuzungumzia taarifa ambayo Zeco imeitoa kwa sababu hana mamlaka nayo.

Zaidi alisema wao walikwishatangaza taarifa ya matengenezo ya kituo cha Ubungo ambayo yanahusisha mashine kubwa tatu na uwekaji wa transifoma ya MW 240.

Alisema mashine hizo zinafanyiwa matengenezo baada ya muda wa kufanya hivyo kuwa umefika.

Muhaji aliahidi taarifa zaidi kuhusu matengenezo hayo kuzitoa kesho.

Muhaji alisema kwa upande wa Tanzania Bara hakuna mgawo isipokuwa kuna matengenezo ya mitambo ambayo yanasababisha hasa Jiji la Dar es Salaam kukosa umeme baadhi ya nyakati.

Alisema Kituo cha Ubungo kinategemewa na Kituo cha Dar es Salaam zaidi kusambaza umeme.

“Ndio maana unaweza kuona baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam yanakosa umeme baadhi ya nyakati na si muda wote na kama umefuatilia vizuri katika hizi siku mbili, juzi, jana na leo hali kidogo imeanza kuimarika kutokana na baadhi ya mambo ambayo wataalamu wetu wamefanya.

Mgawo huo kwa upande wa Zanzibar unakuja wakati hivi karibuni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, aliiagiza Tanesco kufuta deni la umeme wanalodaiwa Zeco ambalo ni takribani shilingi bilioni 22.9.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles