27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kanisa Katoliki lafichua jina la mshindi wa urais DRC

KINSHASA, DRC

BARAZA Kuu la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (Cenco), lenye ushawishi mkubwa  nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limesema linafahamu aliyeshinda uchaguzi wa rais ambao ulifanyika Desemba 30 mwaka jana na kuomba Tume ya Uchaguzi (CENI) kutangaza matokeo katika mazingira huru, haki na ukweli.

Baraza hilo limetoa baada ya tume ya uchaguzi kutangaza kwamba italazimika kuchelewa kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita kutokana na hitilafu za kimitambo.

Kanisa hilo limesema sampuli ya wawakilishi ilichapishwa katika vituo vya kupigia kura ambavyo vinawaruhusu kujua jina la rais aliyechaguliwa. Sampuli hiyo ni ya vituo zaidi ya 23,000 kati ya vituo 70,000 vilivyowekwa na Ceni nchini humo.

Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo, msemaji wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Padri Donatien Nshole, amesema si jukumu lao kutangaza matokeo, bali wao ni waangalizi lakini wanafahamu nani aliyechaguliwa na wananchi.

“Ni muhimu kusisitiza kuwa kasoro zilizojitokeza haziwezi kuathiri kwa kiwango kikubwa chaguo la wananchi wa DRC walioonyesha wazi katika uchaguzi wa urais wa Desemba 30. Cenco imeitaka Tume ya Uchaguzi (Ceni) kama taasisi inayounga mkono demokrasia kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa heshima ya ukweli na haki,” amesema Padri Nshole.

Msemaji huyo amekuwa anawasilisha ripoti ya awali ya ujumbe wa waangalizi wa Uchaguzi wa Tume ya Haki na Amani ya Cenco, ambayo inasema kuwa ilikuwa na waangalizi 40,000 siku ya uchaguzi mkuu.

Uchaguzi huo utapelekea kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye hakuruhusiwa kuwania muhula wa tatu kulingana na Katiba.

Mwanzoni mwa wiki hii Tume ya Uchaguzi, Ceni ilisema itatangaza matokeo ya awali Januari 6, mwaka huu, kabla ya siku chache baadaye kubadili kauli kuwa huenda zoezi hilo litaahirishwa.

Raia nchini DRC bado wanasubiri kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo. Hali ya wasiwasi bado inaendelea, huku huduma ya intaneti ikiendelea kufungwa na mitambo ya radio ya kimataifa ikizimwa. Wakati huo Ceni imesema tayari imehesabu asilimia 20 tu ya kura zilizopigwa.

Kwa upande wake Serikali ya Marekani imeiomba Ceni kutangaza matokeo sahihi na kusema yeyote atakayekwenda kinyume na demokrasia ya nchi hiyo atawekewa vikwazo. Marekani pia imeitaka Serikali ya Congo kufungua mtandao wa intaneti na kuondoa vikwazo kwa vyombo vya habari.

Shirika la utangazaji la Ufaransa, RFI, ambalo lina wasikilizaji wengi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, linasema mwandishi wake, Florence Morice, alilazimika kuondoka nchini humo baada ya kibali chake cha kufanya kazi kufutiliwa mbali.

Uongozi wa DRC kupitia Waziri wa mawasiliano, Lambert Mende, unalituhumu shirika hilo kwa kuleta utata baada ya kutangaza matokeo yasiyo rasmi madai ambayo shirika lenyewe limekanusha.

“Ni muhimu kufahamu kwamba chini ya sheria za Congo, ni Ceni pekee yenye mamlaka ya kuandaa uchaguzi na kutangaza matokeo,” alisema Mende.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilitarajiwa kufanya mkutano wa faragha kujadili uchaguzi wa DRC. Mkutano huo umeitishwa na Serikali ya Ufaransa, wakati ambapo mataifa yenye nguvu duniani yanasubiri matokeo ya uchaguzi huo.

Tume ya uchaguzi imepanga kutangaza matokeo kamili Januari 15 na rais aliyechaguliwa ataapishwa siku tatu baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles