27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za Serikali.

Mabadiliko hayo aliyafanya jana na kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Ikulu Dar es Salaam.

 Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Waziri wa Madini, Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji.

Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli amefanya uteuzi wa waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji, hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pamoja na hilo, alisema pia Rais Magufuli amemteua Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Madini.

“Kufuatia uteuzi huo, Wizara ya Madini sasa itakuwa na Naibu Waziri mmoja ambapo Mheshimiwa Stanslaus Nyongo anaendelea na wadhifa wake,” alisema Balozi Kijazi.

MAKATIBU WAKUU

Mbali na hilo, alisema Rais Magufuli amemteua Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

“Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu.

“Rais Magufuli amemteua Dk. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo Dk. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (afya),” alisema.

Balozi Kijazi alimtaja Elius Mwakalinga kuwa Katibu Mkuu Ujenzi ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na anachukua nafasi ya Mhandisi Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI.

“Rais Magufuli amemteua Bi. Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Mwingine aliyeteuliwa ni Dk. Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Rais Magufuli amemteua Dk. Francis Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),” alisema.

UBALOZI

Kijazi alisema kuwa Rais Magufuli amemteua Dk. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya). Kituo chake cha kazi kitatangazwa baadaye.

UTEUZI WA RAS

Alisema mkuu huyo wa nchi amemteua Profesa Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Athumani Diwani ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Alisema uapisho wa viongozi hao utafanyika leo saa 3:30 asubuhi, Ikulu Dar es Salaam.

NAFASI KUFUTWA

Balozi Kijazi alisema kuwa Rais Magufuli ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa nchi amefanya uamuzi wa kufungua ubalozi mpya wa Tanzania nchini Cuba na balozi atateuliwa baadaye.

MABADILIKO MWAKA JANA

Novemba 11, mwaka jana Rais Dk. John Magufuli, alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kutengua uteuzi wa mawaziri wawili wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Mbali na kutengua uteuzi wa mawaziri hao, Rais Magufuli aliwapandisha naibu mawaziri wawili kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wizara naibu waziri mmoja huku akiwateua naibu mawaziri watatu wapya akiwamo Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

Waliopandishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye sasa amekuwa Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Tizeba.

Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Kakunda aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji akichukua nafasi ya Mwijage.

Mbali na Waitara aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Kakunda, mwingine ni Constantine Kanyasu ambaye aliteuliwa kuwa Naibu  Waziri wa Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Hasunga.

Pia Innocent Bashungwa aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Mary Mwanjelwa ambaye amepelekwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles