24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo usikubali Tarura wakuangushe

LEONARD MANG’OHA

Hivi karibuni gazeti moja la kila siku liliripoti habari ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kunusa harufu ya ufisadi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Jafo alimtaka Mkurugenzi Tarura, Abdul Digaga, kuwasilisha taarifa za makusanyo ya mapato ya halmashauri na majiji yote nchini ndani ya siku saba kuanzia siku ya agizo hilo.

Aidha, alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika ofisi za Tarura Mkoa wa Dar es Salaam na kubaini kuwapo kwa upotevu wa zaidi ya Sh milioni 200 zilizotakiwa kukusanywa na Tarura katika jiji hilo ndani ya siku sita kuanzia Februari Mosi hadi 6, mwaka huu, hata hivyo zilikusanywa Sh. milioni 24 tu.

Jafo pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamhanga, kufuatilia kwa karibu suala hilo na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa Idara ya Ununuzi ya Tarura waliohusika katika uzembe huo.

Kwa wastani, kila siku Tarura walipaswa kukusanya Sh milioni 39, kwa siku sita wangekusanya Sh milioni 234, lakini katika kipindi hicho cha siku sita, Tarura walikusanya Sh milioni 24.

“Huu ni uzembe wa hali ya juu, kwa siku sita Tarura mmepoteza zaidi ya Sh milioni 200, ambazo mlipaswa mzikusanye kwenye maegesho ya magari. Namwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tarura awasiliane na Katibu Mkuu Tamisemi asimamie jambo hili kwa sababu utendaji kazi wa Idara ya Ununuzi ya Tarura hauko vizuri, wahakikishe wanafanya uamuzi sahihi kwanini Tarura inaharibu” anasema Jafo.

Kaimu Mkurugenzi wa Tarura, Francis Mwasota, anasema sababu ya kutokusanya mapato hayo ni mzabuni aliyepewa tenda hiyo kampuni ya M/S Climate kushindwa kutekeleza baadhi ya mambo waliokubaliana katika mkataba walioingia na Tarura.

Huu ni upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali, upotevu ambao haupaswi kuendelea kuvumilika, hivyo hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya watumishi wote waliohusika na upotevu huo ili kukomesha uzembe huu.

Mwenendo huo unaweza kusababisha upotevu wa takribani Sh milioni 800 kwa mwezi mmoja.

Kwa maneno mengine, mwenendo huo unaweza kuisababishia Serikali upotevu wa zaidi ya Sh bilioni tisa kwa mwaka mmoja. Huu ni uzembe mkubwa kwa wakala huu wa Serikali ulioanzishwa kwa lengo la kuendeleza na kusimamia barabara za vijijini na mijini ambazo awali zilikuwa zikitekelezwa chini ya usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kuanzishwa kwa wakala huu pia kumelenga kuhakikisha, barabara za vijijini na mijini zinapitika kwa urahisi vipindi vyote vya mwaka, kupunguza gharama za matengenezo kwa vyombo vya moto vinavyotumia barabara hizo na kupunguza muda wa safari kutoka eneo moja hadi jingine.

Pia ni kuhakikisha kunakuwa na usalama wa barabara zenyewe na mazingira yake. Taarifa zinaonesha kuwa utafiti uliofanywa na Tamisemi hivi karibuni kila mwaka ni wastani wa asilimia 30 tu ya barabara za vijijini na mijini ndizo hukamilika. Hii inamaanisha kuwa asilimia 70 ya barabara hizo hushindwa kukamiliki.

Kushindwa kukamilika kwa barabara hizo husababisha kutopitika kwa urahisi kwa baadhi ya vipindi vya mwaka hususan msimu wa mvua hali inayokwamishwa shughuli za wananchi kufanyika hivyo kukwamisha juhudi zao za kujiongezea kipato na kupunguza umaskini kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa wamiliki wa vyombo vya moto vipindi hivyo hugeuka machungu kutokana na gharama kubwa za matengezo ya vyombo vyenyewe, ongezeko la matumizi ya mafuta na upotevu wa muda.

Upotevu wa fedha hizi unaashiria nini? Bila shaka ndiyo chanzo cha kutokamilika kwa barabara nyingi kutokana na ufinyu wa bajeti inayotekeleza. Ndiyo, kwa sababu kama mamlaka kama hizi zinashindwa kukusanya fedha kikamilifu ni wazi kuwa hata wakati wa kutenga bajeti pia zitapewa kiasi kidogo ikilinganishwa na taasisi zinazokusanya fedha.

Upotevu huo umeonekana Dar es Salaam pekee, vipi katika mikoa mingine, huko ambako watumishi si wengi, huenda huko hali ni mbaya zaidi.

Tunatambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali za kimkakati na zisizo za kimkakati. Sina hakika kama watendaji wa ngazi za chini wanaliona hili ili kuhakikisha wanaisaidia Serikali Kuu kufikia malengo yake.

Mathalani fedha hizi zilizopotea kwa siku sita tu zingesaidia kwa kiasi gani kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya, elimu, maji na maeneo mengine mengi.

Yawezekana zingesaidia kupunguza adha ya madawati katika shule za Serikali ambazo zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa wanafunzi, au hata zingetumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Vile vile fedha hizi zingesaidia kuchangia katika mfuko wa barabara ili kuwezesha ujenzi wa barabara zinazounganisha wilaya na wilaya au mkoa na mkoa na kurahisisha mawasiliano katika jamii.

Tatizo kubwa linalokwamisha haya ni watumishi wa idara mbalimbali za Serikali kuendelea kufanya mambo kwa mazoea, pasi kuzingatia weledi wala kutaka kubadilika kimtazamo ili kuendana na mabadiliko ya ukuaji wa sayansi na teknolojia pamoja na mabadiliko ya kiuongozi.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles