24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

FELIX TSHISEKEDI Rais mteule anayeweka rekodi ya kidemokrasia

NA MARKUS MPANGALA

MAHAKAMA ya Katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imethibitisha pasi na shaka ushindi wa mgombea urais wa chama cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Felix Etienne Tshisekedi, ambaye amewashinda mgombea wa muungano wa upinzani, Martin Fayulu, aliyepata kura takribani milioni 6.4, huku mgombea wa chama tawala cha PPRD (People’s Party for Reconstruction and Democracy), Emmanuel Ramazani Shadary, akipata takribani kura milioni 4.4.

Hii ni mara ya kwanza katika historia yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshuhudia tukio kubwa la kukabidhiana madaraka kwa amani kati ya mtoto wa Etienne Tshisekedi (Felix Tshesekedi) na mtoto wa Laurent Desire Kabila (Joseph Kabila).

Sherehe hizo zilifanyika wiki hii katika makao makuu ya Bunge. Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya mambo ya Nje ya DRC, marais 17 kutoka nchi za Afrika, walihudhuria tukio hilo la kihistoria. Ufaransa na baadhi ya nchi kadhaa za Ulaya ziliwakilishwa na mabalozi wao.

Hata hivyo, marais wawili wa nchi jirani, Paul Kagame (Rwanda) na Edgar Lungu (Zambia), hawakuhudhuria sherehe hiyo.

Zoezi hilo la kukabidhiana madaraka limehitimisha miaka 18 ya utawala wa Joseph Kabila Kabange, ambaye alichukua madaraka baada ya kifo cha baba yake, Laurent Desire Kabila (Mzee) ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi katika Ikulu ya Kinshasa Januari 16, mwaka 2001.

Felix Antoine Tshilombo Tshisekedi, anakuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akichukuwa mikoba ya mtangulizi wake, Joseph Kabila, ambaye anamaliza muda wake.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya nchini humo, Ceni, ilitangaza kuwa Felix Tshisekedi, alishinda uchaguzi kwa asilimia 38, na kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba.

Hata hivyo, Martin Fayulu, mgombea urais mwingine wa upinzani aliyeshindwa, ambaye anaendelea kudai kuwa alishinda uchaguzi huo licha ya kuibiwa kura, amesema kamwe hatamtambua Felix Tshisekedi kama rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Haya yanaweza kuitwa mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jumla ya wapigakura milioni 46 waliojiandikisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), walitakiwa kushiriki zoezi la uchaguzi mkuu la kuwapigia kura wagombea 34,900 katika viti 500 vya kitaifa, viti 715 vya mikoa na 21 vya urais na vituo 21,100 vya kupigia kura kote nchini humo katika uchaguzi uliofanyika Desemba 30, mwaka jana.

Felix Tshisekedi ni nani?

Jina lake kamili ni Felix Ettiene Tshisekedi. Ni kiongozi wa Chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS).

UDPS ni chama kikongwe zaidi cha upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tshisekedi aliidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa pamoja baada ya mazungumzo kati yake na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation), Vital Kamerhe.

Mwafaka kati ya wawili hao uliafikiwa jijini Nairobi mnamo Novemba 23, mwaka jana baada ya kushindikana kuwa mgombea wa muungano wa upinzani nchini humo.

Felix Tshisekedi ni mtoto wa mwanzilishi wa chama cha UDPS, mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu, Etienne Tshisekedi.

Baba yake alifariki dunia Februari mwaka 2017 na sasa mtoto wake akitumia umaarufu wa mzazi wake kuombea kura za urais, sasa anatarajiwa kukabidhiwa jukumu la kuongoza DRC ambayo imekuwa kwenye mgogoro wa kivita na demokrasia kwa kipindi kirefu.

Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55, mnamo Novemba 11 mwaka jana akiwa na Vital Kamerhe pamoja na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Martin Fayulu apambane na Emmanuel Ramazani Shadary.

Makubaliano yao yalidumu saa 24 pekee. Tshisekedi na Kamerhe walidai kushinikizwa na vyama vyao kujiondoa na wakajitenga na Fayulu hatua iliyougawa upinzani.

Makubaliano yao yalikuwa kwamba wakishinda, Tshisekedi atakuwa rais na Kamerhe, ambaye ni rais wa zamani wa Bunge na ambaye aliwania dhidi ya Joseph Kabila mwaka 2011 atakuwa na madaraka ya uwaziri mkuu.

Tangu baba yake alipoanzisha chama cha UDPS mwaka 1982, kilikuwa kama chama kikuu cha upinzani, mwanzoni wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko, kisha wakati wa utawala wa Laurent-Desire Kabila, aliyeongoza tangu mwaka 1997 hadi kifo chake 2001.

Felix Tshisekedi alizaliwa jijini Kinshasa mnamo Juni 13, mwaka 1963 kwa wazazi wake Martha na Etienne Tshisekedi. Baba yake ametokea kabila la Luba.

Wakati baba yake alipoanzisha chama cha upinzani cha UDPS kupambana na Mobutu, ilimlazimu Felix kuambatana naye siku moja baada ya kukamatwa na vyombo vya dola. Hilo lilichangia Felix kuachana na elimu.

Mwaka 1985, Felix aliruhusiwa na Serikali ya Mobutu kuondoka kijijini Kasai na kwenda kuishi jijini Brussels nchini Ubelgiji ambako alifanya kazi mbalimbali ili kujikimu kimaisha.

Baadaye alikuwa miongoni mwa wapiganaji wa kikosi cha chama hicho cha UDPS. Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Mahusiano ya kimataifa wa chama hicho.

Mwaka 2011 alifanikiwa kushinda nafasi ya ubunge akiwakilisha Mkoa wa Mbuji Mayi uliopo katika Jimbo la Kasai. Mnamo Oktoba mwaka 2016, alichaguliwa Naibu Katibu mkuu wa chama cha UDPS.

Machi 31, mwaka jana alichaguliwa kuwa kiongozi wa UDPS baada ya kifo cha baba yake kilichotokea Februari mosi mwaka 2017. Machi 31, mwaka jana alichaguliwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu uliopita.

Mawili mazito yanamkabili Tshisekedi

Yapo mambo makubwa mawili ambyo yanamkabili kiongozi mpya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mambo ambayo yanatakiwa kusimamiwa kwa udi na uvumba.

Kwanza, nchi hiyo inahitaji amani na usalama kama msingi wa kurudisha utulivu wa nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na vita ya mara kwa mara kutoka kwa makundi mbalimbali ya waasi.

Ni zaidi ya miaka 20 sasa hali ya usalama na utengamano haujawa wa kuridhisha DRC. Changamoto kubwa ni kuangalia vipi Tshisekedi anaweza kuleta amani kwa taifa hilo hususan eneo la Mashariki ambako kumeshuhudia ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia na uwepo wa wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

Pili, nchi hiyo ina utajiri mkubwa lakini raia wake ni masikini wa kutupwa ikizingatiwa mfumo mzima wa utawala nchini humo una miongo mingi.

Pia anatakiwa kwa kutazama na kutathmini ukubwa wa nchi yenyewe na uwezo wa Serikali kuweza kukidhi mahitaji ya raia wake.

DRC, kwa ukubwa wake, uchumi wake umegubikwa kwa ukosefu wa miundombinu msingi. Licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali, Benki ya Dunia inasema takribani 63% ya idadi jumla ya raia nchini humo wanaishi katika umasikini.

DR Congo ina utajiri wa madini kama vile shaba, almasi zinc, mafuta, dhahabu na kadhalika. Lakini licha ya utajiri huu wote, bado maisha ya raia nchini humo ni duni.

Hakuna njia nyingine ambayo inaweza kuibadilisha DRC kama kuweka usalama na amani pamoja na kuinua uchumi. Mambo haya mawili ndiyo makubwa na nyeti mno katika utawala wa rais mpya.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles