28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dilunga anavyohaha kumuenzi baba mkubwa

ZAINAB IDDY

KATI ya usajili makini wa wachezaji wa ndani uliofanywa na Klabu ya Simba msimu huu ni wa kiungo Hassan Dilunga.


Simba ilimsajili Hassan Dilunga ikilenga kuimarisha sehemu ya kiungo ya timu hiyo inayopambana kutaka kuandika rekodi mpya katika medani ya kimataifa.

Hassan ameongeza utamu katika eneo la kiungo la Simba ambalo pia lina wachezaji wengine mahiri, akiwamo Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Haruna Niyonzima, Jonas Mkude,  James Kotei na raia wa  Zambia, Clatous Chama, ambaye amesajiliwa msimu huu.

Ni wazi katika kundi hili la viungo, mpaka sasa waliofanikiwa kupata nafasi ya kucheza ni Chama, Hassan, Mkude na Kotei.

Hassan, ambaye alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar, ambako alikuwa mchezaji muhimu, ameonyesha ukomavu na mchango wa maana kwa timu yake hiyo si tu katika Ligi Kuu Tanzania Bara, pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akiiwezesha kutinga hatua ya makundi.


Uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira na kutoa pasi zenye macho umemfanya Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, kujenga imani naye na kumpa nafasi ya kutosha katika michezo ya timu hiyo.

Jambo zuri zaidi kwake ni kujiamini mno alikonako, lakini pia anajikubali, hasa kile anachokifanya uwanjani, jambo ambalo linamsaidia kumshawishi kocha ampe nafasi.

Tunaweza kusema  Hassani anasafiria vema nyota ya staa wa zamani wa Yanga, Simba, Pan African na Cargo Star  pamoja na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Maulid Dilunga, ambaye ni baba yake mkubwa.

Maulidi Dilunga ambaye alifariki dunia mwaka 2008, aliichezea Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo, kuanzia mwaka 1964 hadi 1974.


Mwaka 1969, Maulid Dilunga aliiongoza Yanga kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na wachezaji kama Salehe Zimbwe, Hassan Gessan na Kitwana Manara.

Yanga ilitolewa na Asante Kotoko, baada ya kurushwa shilingi baada ya dakika 90 timu hizo kufungana bao 1-1. Huo ulikuwa mchezo wa pili, katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam matokeo yalikuwa sare ya mabao 2-2.

Mwaka 1972, Maulid Dilunga alijumuishwa katika kikosi cha kombaini ya Afrika, akiwa na wachezaji wengine wa Tanzania, Arthur Mwambeta na Kitwana Manara.

Mwaka 1974 alichaguliwa namba 10 wa kombaini ya Afrika akiwa na Mtanzania mwenzake aliyekuwa kipa, Omari Mahadhi (marehemu).

Makali yake ya kucheka na nyavu ndiyo yaliyomfanya achaguliwe katika kikosi cha kombaini ya Afrika, baada ya kumalizika kwa michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Katika kikosi hicho pia alichaguliwa kuwa nahodha.

Kikosi hicho kilizuru mataifa mbalimbali ya Amerika na Ulaya kucheza mechi za kirafiki.

Walifanikiwa kwenda Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru, Hungary na Bulgaria.

Hassan aendeleza makali

Ni ukweli ulio dhahiri, Hassan Dilunga anazidi kuwa bora dimbani kadri anavyopata nafasi katika kikosi cha Aussems, kwani ushahidi ni kile anachokifanya katika Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi

Katika michezo aliyoichezea Simba hadi sasa, Dilunga ameonyesha kuwa ni mtulivu na makini katika kupiga pasi za mwisho ambazo zimekuwa zikitendewa vema na washambuliaji wa Simba.

Wakati anatua Simba hakuna aliyefikiria kwamba Hassani atapata fursa ya kuingia katika kikosi cha wachezaji 11, kwakuwa tayari walikuwapo wachezaji wengine mahiri katika eneo la kiungo la timu hiyo.

Lakini ameweza kupenya katika kizuizi kikubwa kilichomshuhudia Niyonzima akichemka kukivuka.

Makali yake yalithibitika mapema wakati Simba ikiwa katika mechi za maandalizi ya msimu mpya.

Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Arusha United,  alitengeneza nafasi mbili zilizotumiwa na Okwi kufunga mabao.

Pia alitoa pasi makini kwa mshambuliaji Meddie Kagere, ambaye alifunga bao kabla ya yeye kufunga la pili na la ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao ya Jamii.

Kuaminikwa kwake na benchi la ufundi lililo chini ya Aussems kulianzia hapo. Hakika alijaa katika vinywa vya mashabiki na wapenzi wa Simba.

Mwenyewe afunguka

“Tangu awali nilishaweka wazi kuwa nimekuja Simba ili kupata changamoto zitakazonipeleka kucheza soka la kimataifa na kuondoa dhana ya kuwa mimi ni mchezaji wa Morogoro na Dar es Salaam.

“Lakini pia, mara nyingi nimekuwa na kawaida ya kupata nafasi ya kucheza na kung’ara msimu wa kwanza, unaofuata nakosa nafasi na mwisho napotea, hili lilimalizika Mtibwa Sugar.

“Sitaki maisha niliyopitia Yanga yanikute Simba, kwani nina malengo yangu ambayo nataka Nitimize

Lengo langu ni kuliendeleza jina la Dilunga, ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania wakati akicheza soka,” anasema.

 “Kujiunga kwangu na Simba kumebadili sana mfumo wa maisha yangu, ikiwamo ratiba zangu za kila siku.

Kwakuwa kocha anataka tuwe wachezaji wazuri, nalazimika kupunguza hata muda wa kusikiliza muziki, kucheza gemu na kukaa na marafiki na kuutumia kufanya mazoezi.

“Ukiwa hujui nini unafanya unaweza kusema Simba kuna maisha ya ufungwa au ya kishule shule, lakini kwa upande mwingine ni mazuri kwa wachezaji, binafsi nayafurahia na ninawaahidi mashabiki na viongozi wa Simba nitaongeza juhudi ili niwe bora zaidi ya hapa.

“Tayari lengo la kwanza la kurejeshwa Taifa Stars limetimia, kilichosalia ni kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa, hii itanisaidia kurejesha kumbukumbu ya baba yangu mkubwa, Mzee Maulid Dilunga kwa Watanzania,” anasema.

“Nimekuja Simba kufanya kazi, hivyo nitahakikisha natimiza majukumu yangu ya ndani ya uwanja, ikiwamo kutengeneza nafasi na kufunga mabao kwa kila nafasi nitakayopata, zaidi  nahitaji tu kuendelea kuaminiwa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles