30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 500/- zalipwa kwa wakulima wa korosho

MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema zaidi ya Sh bilioni 500 zimelipwa kwa wakulima wa korosho kati ya Sh bilioni 700 zinazotarajiwa na kwamba, malipo hayo bado yanaendelea kulipwa kwa wakulima wengine waliosalia.

Alisema tamko la Rais Dk. John Magufuli la kwamba Serikali itanunua korosho kwa bei ya Sh 3,300 ni kwa ajili ya korosho za daraja la kwanza  na bei ya korosho za daraja la pili ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni jijini Dodoma, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CCM).

Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho ambao walikuwa wakilipwa Sh 2,600 kwa kilo wakati Rais Dk.  Magufuli alisema Serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa Sh 3,300.

“Malipo yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, Serikali itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. Taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha anayelipwa ni mhusika. Wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu,” alisema Majaliwa.

Alisema ilikuwa ni lazima kwa Serikali ifanye uhakiki kwa wakulima hususani wale wenye kilo zaidi ya 1,500 ili kujiridhisha kama ni wakulima, hivyo baada ya kuhakikiwa, wakulima wote watalipwa fedha zao.

Alisema Januari 27, mwaka huu, alitoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wahakikishe hadi Februari 15, mwaka huu wawe wamekamilisha zoezi la uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao kilichofanyika mkoani Mtwara, lengo likiwa ni kupata taarifa juu ya mwenendo mzima wa bidhaa hiyo kwa msimu wa mwaka 2018/2019.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali haijakiuka sheria kuhusu suala la watumishi kupandishwa mishahara na kwamba ina nia njema ya kuhakikisha wanalipwa mishahara na posho nzuri.

Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga, aliyedai Serikali imekiuka sheria ya utumishi kwa kutopandisha mishahara, ambapo Waziri Mkuu alisema  Serikali haikukiuka sheria, bali iliamua kushughulikia suala hilo kwa kuanza na uhakiki wa watumishi.

Alisema baada ya kufanya uhakiki na kubaini uwepo kwa watumishi hewa pamoja na waliokuwa wakitumia vyeti vya kughushi, iliwaondoa na sasa Bodi ya Mishahara na Masilahi ya Watumishi wa Umma inafanya mapitio ya mishahara baada ya kubaini tofauti, hivyo watumishi waendelee kuwa watulivu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles