23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Saa 12 mikononi mwa magaidi

NAIROBI, KENYA

NANCY ni miongoni mwa walionusurika katika shambulio la kigaidi kwenye majengo ya Hoteli ya Dusit D2, iliyopo Riverside, baada ya kukaa ndani kwa saa 12 huku akisubiri msaada wa kuokolewa.

“Shambulizi lilitukuta tukiwa tunamalizia mkutano katika ofisi zetu zilizopo Riverside siku ya Jumanne, Januari 15, ilikuwa kama saa 9 alasiri. Kichwani nilikuwa na jambo moja tu, kukimbilia nje na kuendesha gari kwa kasi bila kujali taa za barabarani na kufika nyumbani ili kuwahi kumpokea mwanangu getini baada ya kushushwa na gari la shuleni kwao.

“Tulikuwa tunaagana na wenzetu wakati tuliposikia mlipuko kutoka upande wa pili wa mto. Uamuzi wa haraka uliochukuliwa na wenzangu ni kukimbilia dirishani. Lakini kutokana na mafunzo yangu ya ulinzi, niliwaonya juu ya tabia kama hiyo ya kukimbilia dirishani.”

Mmoja wa wafanyakazi wenzake alisema ana mtoto anayesoma Shule ya Consolata, ambayo ili kuifikia ni lazima kuvuka mto huo na alitakiwa kuhakikisha kuwa mtoto wake yuko salama.

“Tuliamua kutoka nje ya chumba cha mikutano na kuondoka. Lakini walinzi walituonya kuwa watu wanakimbilia nje ya jengo.”

Shambulizi

“Hapo ndipo nilipogundua kuwa tumeshambuliwa. Nilikimbia tena ndani na kuchukua mkoba wangu, lakini wakati nakimbilia kule juu, kulikuwa na sauti isiyo ya kawaida, kulikuwa na mkanganyiko. Vijana na wazee, wagonjwa na wenye afya njema walikuwa wanasukumana wenyewe kwa wenyewe ili kupata upenyo wa kujiokoa na kukimbilia nje ya majengo.

“Upesi nilianza kupiga kelele, kuwaomba watu wasisukumane na wala wasikimbie. “Tutatoka nje sote pamoja, niliwaambia. Tukaweka mkakati wa namna ya kutoka nje, kwanza tulikubaliana kuwatanguliza wazee na wanawake wajawazito.

“Kutoka kwenye ghorofa ya pili tuliona magaidi wawili kupitia dirishani. Walishika silaha nzito sana. “Nikawaonyesha: “Haya, ndiyo wale hebu waone.

“Ilitokea kama ajali tu, gaidi mmoja aliangalia kule juu na macho yetu yakakutana ana kwa ana. Akaelekeza bunduki yake kwenye kundi tulilokuwepo na kushambulia. Risasi zilitoboa dirisha na kuvunja kabisa.”

Maombi

“Wote tulisambaratika. Nilijikuta nimejificha chini ya meza wakati risasi zikirushwa hewani zikipasua madirisha. Ilikuwa hatari sana.

“Nilimpigia simu mama yangu na kumwambia tunashambuliwa na magaidi na nikamwomba atuombee. Nikaanza kujifikiria mwenyewe nikiwa nimezungukwa na ndugu zangu na nikagundua kuna soketi ya umeme. Bahati nzuri nilikuwa na chaja ya simu. Haraka nikachomeka na kutoa mlio kwenye simu yangu. Nikaanza kutuma meseji kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp kuwaambia watu kuwa tunashambuliwa na magaidi.

“Muda huo huo nikasikia mlio wa risasi na mlipuko ukatokea. Wakati mwingine sauti ya mlipuko ilikuwa karibu sana, nikajisemea mwenyewe, sasa nimepatikana.

Lakini nilikuwa napokea meseji nyingi za kunipa pole na kunipa moyo.”

Kuokolewa

“Tuliendelea kufanya mawasiliano na kwa kiasi kikubwa maofisa usalama waliwasiliana nami kutaka kujua eneo halisi nililokuwepo. Niliwaelekeza eneo nililokuwepo na walinihakikishia kuwa watakuja kuniokoa. Walituomba tusiwe na papara, wakataka tuwe watulivu.

“Ilipofika saa 4 usiku, umeme ulikatwa. Nilipiga simu kwa mmoja wa maofisa usalama kuuliza kwanini umeme umekatwa na kwa mara nyingine alinihakikishia nisiwe na wasiwasi na akasema watatumia giza hilo kutuokoa wote.

“Ilipofika saa 5 usiku, nilisikia sauti na kujaribu kujificha ndani zaidi kwa nafasi iliyobaki, nilifikiria kuwa watakuwa karibu yangu tayari kuniua. Lakini nikasikia, polisi, polisi, polisi, hapo ndipo nami nikatoka nje na kuamini kuwa wamenifuatilia kwa mawasiliano yangu.

Kitu cha kwanza walichosema: “Jitambulishe mwenyewe,” hilo nililifanya bila wasiwasi. Waliniuliza idadi ya watu waliokuwa nami na kama naweza kuwabaini wote. Kisha walinichukua na kunizunguka wakati wakinisaidia.

“Walikuwa na silaha zilizokokiwa kabisa na kuzielekeza kila kona, wakati naelekea kuwaonyesha maeneo mengine waliyojificha wenzangu.

“Baada ya hapo walituhamisha na kutuweka katikati ya jengo na kusema tubaki hapo pamoja na kukaa mbali na madirisha ya jengo hilo na watakuja tena kutuondoa baada ya kuhakikisha usalama wa majengo yote.

“Tulikaa hapo kwenye maficho kwa masaa manne, lakini kikosi cha maofisa usalama kiliendelea kuwasiliana na sisi, kutuambia tuwe wavumilivu na watulivu, pale tutakaposikia mlipuko wowote au sauti za risasi kwa sababu watakuwa ni wao polisi wakipambana na magaidi kuhakikisha wanakomboa jengo zima.

“Kikosi kingine tofauti kilikuja kutuokoa saa 9:45 alfajiri. Hapo ndipo nilipokuja kuelewa hali halisi. Maofisa hao walitueleza kwa ufupi kilichotokea.

“Walituambia kuwa kama tungekuwa tunapita sehemu yenye dirisha, tuhakikishe tunapita kwa kasi, kisha tupunguze mwendo baada ya kupita na kujificha katika nafasi na kutoka nje kwa kasi kubwa.

“Askari hao walitembea kwenye ghorofa ya pili kwenda ya chini katika mlango wa dharura, huko ndiko waliegesha magari yaliyokuja kutuokoa.

“Walituzingira kwa bunduki kwa kila upande na walitembea na kukimbia wakiwa wameinama. Pia walituambia kuhakikisha kuwa tusiwe na papara.

“Hata pale tulipokuwa ndani kusubiri kuokolewa, wakati wote walituonya kuacha papara. Tulifanikiwa kutoka nje tukiwa pekupeku.

Sikujua kama nakimbia kwenye sakafu ambayo ilijaa vipande vya vioo, kwani sikujisikia maumivu yoyote.

“Tulichukuliwa na kupelekwa kwenye kituo cha Msalaba Mwekundu na kupewa ushauri kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

“Tulikutana na ndugu na familia zetu nje wakitusubiri, hatimaye nikafanikiwa kufika nyumbani asubuhi. Nilichojifunza katika shambulizi hilo ni umuhimu wa kuwa na mtandao mkubwa wa watu kimawasiliano. Nilikuwa na marafiki na ndugu zangu ambao walikesha usiku wote kuniombea.

“Wengine walikuwa wanatoa taarifa kila baada ya muda kuelezea kinachoendelea baada ya kutazama runinga na kutuona tukikimbia kutoka upande mmoja kwenda mwingine katika tukio halisi.

Wengine walikuwa wanawasiliana kwa meseji ili kuhakikisha wanapata taarifa zangu na kuchukua tahadhari kwa kuandika jina langu ‘Nancy’ na hayo yote yalinisaidia kuokolewa na kuwa watulivu.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles