24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Nigeria wamchagua Rais mpya mabomu yakirindima

LAGOS, NIGERIA

HATIMAYE wananchi wa Nigeria jana walishiriki katika zoezi la uchaguzi mkuu wa urais la kumchagua rais mpya wa kuliongoza taifa hilo lenye watu milioni 190 na wawakilishi wa bunge, huku vituo zaidi ya 120,000 vikifunguliwa majira ya saa mbili kamili kwa saa za Nigeria na kushuhudia maelfu ya raia wakimiminika kwenda kwenye vituo hivyo kupiga kura.

Uchaguzi huo umefanyika baada ya kuahirishwa kwa wiki moja baada ya kutofanyika jumamosi wiki iliyopita nchini humo kutokana na kile ambacho Tume ya Uchaguzi ilikiita kutokamilika kwa maandalizi ya tukio hilo.

Wapiga kura nchini humo wanapaswa kuwachagua wawakilishi 360 watakaoingia katika bunge na maseneta 109 ambapo wagombea wa nafasi zote hizo wapo jumla ya 65,000. Matokeo ya awali ya uchaguzi yanatarajiwa kuanza kutolewa kuanzia kesho ambapo mshindi ataongoza taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kwa miaka minne ijayo.

Vyombo vya habari nchini Nigeria vimeripoti kuwa zoezi la uchaguzi mkuu nchini humo limefanyika jana huku baadhi ya watu wakiwa na wasiwasi mkubwa wa kujitokea vituoni na kujiweka kwenye hatari ya kushambuliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Awali Rais Muhammadu Buhari aliwataka wananchi wa Nigeria wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura. Katika uchaguzi huo ulioahirishwa wiki iliyopita Rais Buhari alipambana na mfanyabiashara Atiku Abubakar ambaye hapo awali alikuwa makamu wa Rais.

Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria wiki iliyopita iliahirisha uchaguzi huo wakati Wanigeria zaidi ya milioni 72 walipokuwa wanajitayarisha kwenda kupiga kura.

Akilihutubia taifa kwenye televisheni juzi, Rais Buhari aliwataka Wanigeria wasiwe na wasiwasi na wawe na imani kwamba tume ya uchaguzi itatimiza jukumu lake. Naye mshindani wake kiongozi wa chama kikuu cha upinzani PDP Atiku Abubakar alitoa wito huo huo kwa wapiga kura.

Zaidi ya Wanigeria milioni 84 wameandikishwa kupiga kura kwenye taifa hilo lenye watu milioni 190 la magharibi mwa Afrika. Lakini kwenye maeneo mengi ya kaskazini, ambako uasi wa kundi la Boko Haram umesababisha vifo vya zaidi ya watu 27,000 na kuwafanya mamilioni kuyakimbia makazi yao. 

Kulikuwa na wasiwasi kuwa maelfu ya watu huenda wasiweze kushiriki kwenye uchaguzi wa jana. Wananchi wa mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo wamekuwa wakilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na kundi la kigaidi la  Boko Haram, hivyo kukosa hamu ya kupiga kura ingawa wanatarajia matokeo ya kura hiyo yatarudisha tena amani kwenye maeneo yaliyotawaliwa na matumizi ya nguvu.

Wakati huo huo, jana saa chache kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura, kumeripotiwa mfululizo wa milipuko kaskazini mashariki mwa mji wa Maiduguri, mlipuko ambayo imeripotiwa kutekelezwa na wapiganaji wa kundi la kiislamu la Boko Haramu.

Katika uchaguzi huoRais Muhammadu Buhari alikuwa miongoni mwa raia wa awali kabisa kupiga kura ambapo alifanya hivyo katika mji wa Daura, Kaskazini magharibi mwa jimbo la Katsina ambapo amesema anaamini atashinda uchaguzi huu.

Mpinzani wake wa karibu Atiku Abubakar naye alipiga kura kwenye jimbo lake la nyumbani la Adamawa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles