30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM tusaidie ardhi yetu Misenyi

MWANDISHI WETU

WANANCHI wa Misenyi mkoani Kagera, wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutokana na eneo lao kuchukuliwa na uongozi wa wilaya hiyo.

Wananchi hao wamekuwa na malalamiko yao zaidi ya miaka 12 chini ya mwanakijiji wa familia ya marehemu, William Mabagara wa Bunazi.

Kutokana na hali hiyo, anasema endapo rais akiingilia kati ndiyo inaweza kuwa njia pekee ya kupata eneo hilo kutokana na kufikisha suala hilo kwa ofisa ardhi, mkurugenzi wa Halmashauri ya Missenyi, Mkuu wa Wilaya Missenyi,  Mkuu wa Mkoa Kagera, Kamishna wa Ardhi wa Kanda ya Ziwa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ofisini kwa Waziri Mkuu, lakini mambo bado ni magumu.

Anasema aliwasilisha barua katika maeneo kwa ajili ya kupata msaada, lakini baadhi ya watendaji husika na wengine amekutana nao ana kwa ana, utekelezaji wake umeshindikana katika kipindi chote hicho.

Anasema vielelezo vyote muhimu kama vile majibizano ya barua mbalimbali na ramani kwa uthibitisho kama familia  anavyo, lakini anashangaa kuona suala hilo halipati ufumbuzi.

Anasema suala hilo kutohitimishwa na mamlaka alizozitaja hapo juu, kama familia waliafikiana kumwandikia barua Rais Dk. John Magufuli kumbukumbu namba WM/2018/02 ya  Februari 5, 2018 ambayo ilitumwa ofisini kwake Februari 7, 2018 kwa njia ya EMS namba yenye EE201416321TZ.

Anasema kwa kuwa Rais Dk. Magufuli amekuwa akisisitiza kwa nyakati tofauti, hasa anapokuwa ziarani mkoani kama vile Njombe, alielekeza mamlaka ya kiserikali ikimkuta mwananchi mahali na ikatwaa ardhi yake, basi mwananchi husika anastahili fidia kwa mujibu wa sheria za ardhi.

Na endapo mwananchi atavamia ardhi ya mamlaka fulani ya kiserikali, basi mwananchi huyo hatastahili fidia.

Anasema wao kama familia, wazazi wao wameishi Bunazi Missenyi tangu mwaka 1962, marehemu baba akiwa mtumishi wa Serikali (mwalimu wa shule ya msingi) na mkulima.

Anasema wamekuwa katika eneo hilo na kusomea elimu ya msingi hapohapo hadi baba yao alipofariki dunia kwa ajali ya meli ya Bukoba mwaka 1996.

Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi imewakuta hapo na wanaamini wanastahili fidia stahiki na kwa wakati, badala ya urasimu uliokithiri unaofanywa  na viongozi husika.

Anasema wana mashaka kuhusu mchakato wa utwaaji wa ardhi ya familia na ucheleweshaji wa fidia kwa muda wote huo.

Anasema Agosti 2008, halmashauri ilifanya uthamini ya mwanzo na wa pekee wa eneo hili la familia kwa jina la Msiranga Mabagara (mdogo wangu) kwa niaba ya familia na thamani halisi ya eneo husika na vilivyomo kufikia Sh milioni 114.9 (thamani ya soko kwa mwaka 2008). Katika hali ya kushangaza, uthamini ule ulitelekezwa na halmashauri kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi hadi leo.

Anasema uthibitisho wa kutelekezwa kwa uthamini (valuation) tajwa ni kwambakatika kabrasha la taarifa ya uthamini, ulilopitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali Juni 6, 2009 hakuna mahali popote linaposomeka jina la Msiranga Mabagara.

Taarifa ya uthamini huo iliyotelekezwa na hata ile iliyopitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali, tunazo nakala zake kama familia.

Anasema wao kimsingi kama familia hawapingi kutwaliwa ardhi, bali wanaomba kwa unyenyekevu mkurugenzi wa Halmashauri ya Missenyi azingatie taratibu za utwaaji, ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia stahiki na kwa wakati.

Anasema mamlaka zimekuwa zikidai na kusisitiza  kama familia, wanastahili viwanja 10 tu vya makazi na si vinginevyo!

Jumla ya ukubwa wa eneo la viwanja hivyo kwa pamoja hauzidi mita za mraba 15,000, kati ya mita mraba 83,866 zilizotwaliwa kutoka kwenye ardhi ya familia!

Salio la eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 68,866 hazijulikani atapewa nani kwa matumizi gani! Ikumbukwe pia eneo hili wakati linatwaliwa lilikuwa na mazao mbalimbali ya kudumu na ya muda kama kahawa, migomba, miti ya mbao, msitu wa miti ya nguzo (mikaratusi), miti ya matunda aina anuwai, katani, nyumba ya makazi na mazao mengine kadha wa kadha. Hata stahiki nyinginezo katika mchakato mzima wa utwaaji ardhi zimekuwa ‘siri’! Haziwekwi hadharani kwa familia wala kuongelewa na watendaji wa ardhi wala mkurugenzi katika halmashauri yetu.

Namalizia kwa kukuomba Rais Dk. Magufuli utusaidie kuilekeza mamlaka husika ikiwa ni pamoja na ofisi ya mkurugenzi kwa mujibu wa taratibu, atekeleze ulipaji fidia stahiki ya eneo la familia alilolitwaa mwaka 2007 lenye ukubwa wa mita za mraba 83,866 kama alivyoahidi kama nilivyofahamishwa na Kamishna wa Ardhi kwa barua kumb. Na LD/LZ/34/VOL.II/93 ya Julai 15,2013 kwamba, katika mwaka wa fedha 2013/2014 angelipa.

Mwisho.

Kuna hatari kubwa biashara mitandaoni

Na HASSAN DAUDI

MATUMIZI ya mitandao ya kijamii imekuwa na faida kubwa katika miaka ya hivi karibuni, lakini haimaanishi kuwa hakuna madhara kwa maana ya watumiaji.

Ni kile unachoweza kukiambatanisha na msemo wa kiswahili, kuwa kila chenye uzuri, basi aghalabu huwa na kasoro zake.

Au wahenga waliposema ‘uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti’, msemo unaoshabihiana pia na ule usemao si kila king’aacho ni dhahabu’.

Nikirejea katika hilo la faida, hebu fikiria namna mitandao ilivyo na umuhimu mkubwa katika uendeshaji wa biashara.

Tofauti na hapo awali, sasa ni rahisi kuagiza bidhaa yoyote hapo ulipo, ikifikia hata hatua ya kuletewa ikiwa utataka iwe hivyo.

Hiyo si tu ina faida kwa mteja, pia inapunguza kwa kiasi kikubwa gharama ambazo huenda mfanyabiashara angezitumia kukodisha jengo au kuwafuata wateja.

Ilivyo rahisi kwa sasa, anaweza kuuza na kununua mzigo mpya akiwa anatazama runinga sebuleni kwake. Hakika zipo sababu lukuki za umuhimu wa mitandao ya kijamii.

Huku nikiamini hayo ni mafanikio makubwa kwa sekta ya kiuchumi, safu ya ‘Macho Yameona’ inakwazika na aina fulani ya biashara zinazoendeshwa huko mitandaoni.

Ikiilenga moja kwa moja sekta ya afya, macho yameona hairidhishwi na ‘akaunti’ zisizoeleweka ambazo zinajitaja kuhusika na uuzaji wa dawa au kutoa ushauri wa magonjwa mbalimbali. Ni hatari kubwa!

Na kwa bahati mbaya, utafiti mdogo tu unaonesha kuwa magonjwa ambayo zimekuwa zikijinasibu nayo ni yale yanayowasumbua wananchi walio wengi.

Nikitolea mfano kwa uchache, itoshe kutaja kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa ya zinaa.

Wapo walioenda mbali zaidi, wakijinasibu kupitia akaunti zao kuwa ni mabingwa wa tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Si tu ushauri, pia wamekuwa wakiuza dawa ambazo huhitaji kuuliza juu ya umaarufu wake hapa mjini, ikielezwa kuwa zinatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ni mara nyingi utakuta kurasa hizo za Facebook, Instagram au Twitter zikijitamba kuwa kiboko ya matatizo hayo, huku bado ikiwa hakuna uhakika kama kazi wanazofanya zimethibitishwa na mamlaka husika.

Hatari inayoweza kuonekana kirahisi ni kwamba Tanzania, kama yalivyo mataifa mengine masikini, bado kuna uelewa mdogo juu ya maudhui yanayozalishwa na vyombo vya habari, ikiwamo mitandao hiyo (media illiteracy).

Kwa maana hiyo basi, huenda kati ya watu 100 watakaokuwa wameona tangazo la aina hiyo, asilimia 50 wakajikuta wanaamini katika huduma hizo, jambo ambalo ni hatari endapo wahusika ni wababaishaji tu.

Lakini pia, hebu tujiulize tu, ni rahisi kiasi gani kwa aliyepata ushauri wa tatizo linalomsumbua kwa muda mrefu kufikiria mara mbili juu ya kiwango cha taaluma alichonacho aliyeposti?

Mfano mzuri katika hilo ni mmoja kati ya watu wangu wa karibu ambaye baada ya kuona tangazo la ‘wataalamu’ wa afya ya ngozi, aliwasiliana nao na kisha kuletewa dawa ya chunusi aliyoishia kuimwaga alipogundua kuwa haikuwa ikiondoa tatizo lake licha ya kuitumia kama alivyoelekezwa.

Hapo ndipo unapojiuliza, vipi kuhusu madhara ya ndani ya ngozi endapo kemikali zilizotumika kutengeza dawa hizo ni za ujanjaujanja, kwa maana hazikuthibitishwa na wataalamu wa afya?

Kama ilivyo kawaida yake, safu hii imeonesha, ikiamini kuwa hakuna shaka changamoto hiyo itakuwa imekomeshwa baada ya kukamilika kwa zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole.

Mwisho, msisitizo ni kwamba hakuna ubaya kwa mitandao ya kijamii kutumika kama nyenzo ya kiuchumi, hasa kwa nchi yenye maono ya uchumi wa viwanda kama ilivyo Tanzania.

Lakini sasa, lazima uwapo umakini mkubwa, hasa linapokuja suala la afya au elimu ambazo hakuna ubishi kuwa ndizo silaha muhimu za maendeleo jamii yoyote katika uso wa dunia.

Kuliweka sawa hilo, tukubaliane kuwa hakuna jamii inayoweza kupiga hatua ikiwa sehemu kubwa ya rasilimali watu wake ni wajinga au wagonjwa.

Kwamba maana halisi ya mitandao kurahisisha soko huria isiwe fursa ya wahuni wachache kuziweka rehani afya na maisha ya wengine. Hilo haliwezi kukubalika hata kwa bahati mbaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles