33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ishara ya ndoa inayohitaji msaada

CHRISTIAN BWAYA

INAPOFIKIA hatua kwamba wewe, mwenzako au nyote wawili mnaonekana kukabiliana na tofauti zenu kwa namna inayozidisha tofauti hizo, maana yake ni uhusiano wenu unaelekea ukingoni. Ingawa tunafahamu tofauti ni afya ya uhusiano lakini inapotokea zinakuza nyufa kati yenu, hiyo ina maana kuwa mambo hayaendi sawa.

Baadhi ya tabia hatarishi kwenye uhusiano ni pamoja na kukwepa kujadili mambo yanayohitaji kujadiliwa, aliyekosa kuamua kwa makusudi kuzuia kosa lake lijadiliwe kwa kuibua kosa la mwenzake hali inayoenda sambamba na kutokusamehe.

Lakini pia, ukosoaji unaolenga kuumiza hisia za mwenzako, kurejea makosa ya nyuma mara kwa mara kama namna ya kumdhalilisha mwenzako na tabia ya kufoka, kusimanga, kusema maneno makali yanayomfanya mwenzako ajione hana thamani ni baadhi ya tabia hatari kwenye ndoa au uhusiano.

Tabia hizi ni hatari kwa sababu hujenga ukuta wa kihisia baina yenu na hivyo kuwafanya muwe watu wawili wasiowasiliana kwa amani. Matokeo yake ni kutokutaka kuzungumza, kumkwepa mwenzako kwa makusudi lakini wakati huo huo ukijisikia upweke ndani yako hata pale unapokuwa na mwenzako hali inayoweza kukufanya uanze kufungua moyo wako kwa watu wengine, wakati mwingine ukijisikia vizuri kumsema vibaya mke wako, mume wako au mpenzi wako.

Unapoona dalili kama hizi katika uhusiano wako, ni vyema kuelewa kuwa unaelekea kusiko na usipochukua hatua za haraka, upo uwezekano wa kuachana au kujikuta kwenye uhusiano uliojengwa kwenye misingi ya ghiliba, udanganyifu, uzinzi na aina nyingine za kukosa uaminifu kwenye ndoa yako.

Katika mazingira kama haya, watu wengi huwashauri wana ndoa wakae chini wazungumze kumaliza tofauti zao. Changamoto ya ushauri huu, hata hivyo, ni kwamba inapofikia hatua hii, mwenzako, wewe mwenyewe au basi wote wawili mnakuwa hamna tena msukumo wala sababu ya kuzungumza. Kila mmoja wenu, au mmoja wapo kati yenu anajiona yuko sahihi, anaonewa na kunyanyasika kwa sababu anaamini shida si yeye.

Hufikia mahali watu huona ni afadhali kukata uhusiano na wenzi wao kama namna ya kupunguza matatizo wakati huo huo kutafuta watu wengine wa kuwaambia yale wanayotaka kusikia, kuwafanya wajione hawana hatia, wahisi wanaonewa, wananyanyasika, na kwamba uamuzi wa kujificha kwenye handaki ni sahihi kwa afya ya ndoa.

Uzoefu unaonesha kuwa wakati mwingine huyo anayefanya jitihada za kuweka kiambaza cha mazungumzo na mwenzake, huyo anayefanya jitihada za kufukia udhaifu wake, kumzuia mwenzake kuzungumza ndiye hasa anaweza kuwa chanzo cha tatizo.

Mara nyingine, uzoefu unaonesha kuwa tabia zake zinaweza kuwa ndio chanzo cha mwenzake kuamua kunyamaza ingawa hana amani, mwenzake kuamua kumkwepa ili kuepusha shari kwa sababu kila anapohitaji wazungumze anaishia kuumizwa kwa maneno makali, kubebeshwa lawama na hata kujikuta ‘madhambi’ yake yaliyopita kufukuliwa. 

Aidha, kikwazo cha mazungumzo kinaweza kuwa uwezo wa mmoja wapo kuzungumza zaidi ya mwingine, kutokusikiliza hisia za mwenzake, hali inayomfanya anayetamani mazungumzo kukata tamaa kwa sababu kila anachotaka kukisema kinazimwa mwanzo tu wa mazungumzo.

Mtu kama huyu anaweza kutamani kuzungumza na mwenzake asiweze na hivyo kujikuta akilia mwenyewe, akinung’unika kwa watu wasioweza kumsaidia kwa sababu mhusika ambaye ni mke, mume au mpenzi wake, hana uwezo wa kusikiliza.  Uhusiano mbaya kama huu ni vigumu kutengenezwa kwa mazungumzo kama inavyoweza kushauriwa na watu wanaotoa ushauri huo kwa nia njema kabisa.

Badala yake, tunayo mapendekezo mawili makubwa. Kwanza, ni mmoja wapo kuamua kuchukua hatua za makusudi kurekebisha mambo. Kama tulivyotangulia kuona, mara nyingi wapenzi hupenda kujiweka kwenye upande usio na makosa.

Mmoja wapo akiamua kulipa gharama ya kuvunja mzunguko huu wa kulaumiana na kuamua kubeba lawama kwenye hatua za awali kama namna ya kumpata mwenzake, hiyo inaweza kusaidia hasa kama huyo wa pili ni narcissist. 

Hapa tuna maana ya kuchukua hatua za kumthamini na kumpenda mwenzake bila masharti na kuachana na jitihada za kulipiza kisasi kwa makosa yaliyokwisha kufanywa na mtu asiyetaka kuomba msamaha wala kubadilika. Njia hii ni ngumu na si mara zote huleta matunda kwa sababu wapo watu ambao kwa haiba zao, huwezi kufanya lolote wakalikubali.

Njia ya pili iliyothibitika kuwa na msaada kwa wengi ni kutafuta msaada kwa mtu wa tatu asiye na maslahi na uhusiano wenu. Matatizo yenu yanapofika mahali hamuwezi kuyatatua wenyewe mnaweza kushawishika kumtafuta mzazi au ndugu mwingine mnayemwamini.

Ingawa ushauri wa namna hii ni rahisi kuukimbilia, wakati mwingine unaweza kuwa chanzo cha matatizo mengine kama tutakavyoeleza kwenye makala inayofuata.

ITAENDELEA

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles