31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Asimulia alivyobakwa na kaka yake miaka mitano mfululizo

WAKIISHI katika maeneo tulivu ya Wilaya ya Megenagna mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, wasichana takribani saba wanaonekana wakitoka kwenye makazi maalumu wakiwa wamewabeba watoto wachanga.

Ingawa walikuwa na watoto wachanga, miongoni mwao hakuna yeyote mwenye umri unaofaa kubeba ujauzito, jambo ambalo lingemfanya yeyote anayewaona kuwa na shauku ya kujua nini kiliwasibu.

Mmoja wao ambaye jina lake limehifadhiwa ana umri wa miaka 23. Ni vigumu kumtambua ni nani hasa kwa kumtazama. Ni mpole. Alipokuja kwenye makazi haya, miaka iliyopita, hakuja kutafuta kazi.

Bali kutafuta maficho dhidi ya maumivu ya mwili na ya kisaikolojia aliyoyapitia baada ya kubakwa na kaka yake.

Amejawa na woga wa kuangaliana na au kutazama watu baada ya magumu aliyoyapitia.

“Nilikuwa na maisha magumu na ya huzuni,” anakumbuka kipindi kilichopita.

Licha ya kwamba maumivu yake yalikuwa makali, anashukuru angalau sasa anaweza kuendelea kuishi.

Anasema kuna wakati alihisi kutembea huku akiwa ametazama mbele ilikuwa  haiwezekani.

Msichana huyu kwa sasa anafanya kazi katika nyumba iliyompatia hifadhi baada ya tukio la kubakwa inayoitwa Refuge for Women and Children.

Huwashirikisha watu wengine habari zake akiamini kwa kufanya hivyo itasaidia kuwanusuru wasichana wengine walio katika hatari au mazingira ya kukabiliana na unyanyasaji wa kingono.

Kaka yake mkubwa ambaye alimpeleka mjini na kumwahidi kumsomesha alikuwa polisi.

Alikuwa na umri wa miaka 16 wakati huo na wote waliishi katika nyumba moja aliyopanga kaka yake.

“Kwa sababu nilikuwa mdogo, sikujua mengi na sikuweza hata kuongea wazi. Nilipokuwa nikiwaona watu, nilifikiri wangenidhuru pia,” anaelezea masahibu aliyoyapitia.

Alikuwa akifikiria kwamba watu watagundua siri yake kwa kumtazama tu. Kwa hiyo, taratibu akaacha kwenda shule.

Katika kipindi chote cha miaka mitano walichoishi pamoja, kaka yake alikuwa akimbaka. Katika kipindi hicho alipata ujauzito na kutoa mimba mara kadhaa.

Vitisho kutoka kwa kaka yake, umri mdogo na maumivu havikumwezesha kuongea neno hata moja juu ya hili kwa yeyote.

Hata hivyo, anaeleza kwamba siku walipohamia nyumba nyingine alipata fursa aliyokuwa akiitaka.

Muda mfupi baada ya kuhamia kwenye nyumba mpya, mwenye nyumba aligundua namna alivyokuwa hapendi kuongea na watu na hivyo, akamuuliza: “Ni kwanini wewe ni mwoga wa kuwasogelea watu, huyu ni ndugu yako?”

Maswali yote hayo yalikuwa magumu mno kwake kuyajibu.

Kwa sababu alikuwa anatafuta njia za kutoroka ili kulinda utu wake, hakutaka kumdanganya mwanamke mwenzake, lakini kumwambia ukweli lilikuwa  tatizo jingine lililomuelemea.

Baada ya kufikiria na kuupiga moyo konde, alipata nguvu ya kumweleza mwenye nyumba.

Aliposikia habari yake kutoka kwa binti huyo, mwenye nyumba alishitushwa na kuamua kumpeleka mara moja kwenye kituo cha karibu cha polisi.

Baada ya kuhojiwa katika kituo cha polisi, alichukuliwa na kupelekwa kwenye nyumba ambayo wanawake wenye matatizo kama yake hupelekwa na kupewa mahala salama pa kuishi na msaada wa kisheria.

Kesi ilipofika mahakamani, familia ilifahamishwa kuhusu hali ya mambo ilivyokuwa kwa binti yao lakini cha ajabu walimgeuka na kidai kaka mtu hawezi kufanya jambo kama hilo.

“Kila mtu katika familia yangu, isipokuwa mama yangu walikasirishwa na mimi. Mbaya zaidi iligeuka kwamba mimi ndiye mwenye makosa ilihali ndiye mwathirika,” anasema binti huyo.

Anasema hiyo ilimwongezea woga kutokana na kwamba kituo cha polisi hakipokei wanawake wenye matatizo kama yake.

Anasema hawakuwa watu wa kumsikiliza na bila huruma walimwuliza maswali mabaya kama vile: “Ulikuwa wapi siku zote hizo uje kulalamika leo?

Hii ndiyo hali inayowakumba wanawake wengi nchini humo, ambako vijana wanaona vitendo vya kubaka wasichana ni sifa hivyo, husimuliana vijiweni kila wanapofanya uhalifu huo.

Hivyo basi, wasichana wanalazimishwa na jamii kuamini kuwa kubakwa ni makosa yao.

Watu waliowazunguka huwalaumu kwa mambo wanayodai au kuwasingizia kufanya hivyo, kuwalazimisha wengi kuendelea kujificha na kutosikika.

Hata hivyo, msichana huyu alipata hifadhi ambayo kwa sasa imekuwa ni mahala pake pa kazi na amekutana na wanawake ambao waliwahi kubakwa na kaka, baba na hata babu zao.

Anaeleza kuwa hao wote walilaumiwa na jamii kwa kuambiwa kuwa wao ndio wamesababisha wabakwe.

“Sifahamu mengi juu ya mfumo wa sheria. Lakini kwa yale niliyoyashuhudia, naweza kusema mfumo wa sheria ni mbaya hapa nchini,” anasema.

Anasema mara nyingi wabakaji hutembea huru, na tangu alipompeleka kaka yake mahakamani hakuna matokeo yoyote aliyoyapata na mtuhumiwa yupo huru.

“Nilipata maumivu makali, nikasimama mahakamani bila mafanikio. Afadhali nisizungumzie hili,” anaongeza.

Kutokana na kutoa mimba mara nyingi, alihitaji kupata matibabu tofauti tofauti.

“Baada ya haya yote, niliumia zaidi kisaikolojia. Hasa kwa namna ambavyo familia yangu ilivyopokea taarifa ya kubakwa kwangu, iliniuma mno,” anasema.

Anasema alipokuwa nyumbani, hakuweza kula wala kumwamini mtu yeyote aliyekuwa karibu naye. Alikuwa na ndoto moja tu na ilikuwa ni ya kujiua ili kuondokana na maumivu yote aliyopitia.

Msichana huyo anasema aliweza kuyashinda majaribu baada ya kupata msaada wa kisaikolojia.

Hata hivyo, makazi mapya hayakumpatia tu ujuzi mbalimbali ili kuwezesha kuwa mtu anayejitegemea, bali pia yalimwezesha kujiamini kupitia mafunzo ya Taekwondo ambayo pia yalimnufaisha.

“Wakati watu wanapoumizwa hawahitaji mambo mengi. Mara nyingi huwa hawataki kusikia wala kuwa tayari kuelewa chochote licha ya kwamba kuna watu walio tayari kutoa msaada kwao, binafsi naamini tunahitaji kuwa tayari kusaidiwa,” anasema.

Anasema licha ya kwamba wanawake wengi hawazungumzi wazi, anaamini wapo wengi waliokabiliana na mambo mengi mabaya kuliko aliyoyapitia yeye.

Anasema anaamini kuwa kama jamii isingewapuuza, wanawake hawa wangejifunza kutokana na uzoefu wa aina hiyo.

“Tunapowaona wanawake wamevaa vitambaa na kutembea kana kwamba uzito wa dunia uko kwenye mabega yao, ninadhani pia wanaishi maisha yangu, kwa hiyo huwa nawafuata na kuzungumza nao, kuwasikiliza na kuwakumbatia.

Anasema anaamini kwamba jamii inahitaji kujifunza kuhusu wanawake na masaibu wanayoyapitia ili kuwasaidia.

Anasema hii itawezesha kuzuia mashambulio sawa na hayo.

“Familia zinapaswa kufahamu kuwa mavazi, chakula na masomo, ambayo watoto wao wanapokea havitoshi, wanahitaji kutambua kuwa wanaweza kuwa katika hali ya hatari kokote wanakoenda,”anasema.

Makazi Refuge for Women and Children yamekuwa yakiwasaidia wanawake kisheria na kisaikolojia kwa miaka 15 sasa.

Maria Munir, ambaye ni mwasisi wa makazi hayo, alilieleza Jarida la ‘Temsalet Gets’ nchini humo kwamba hakuna chochote kinachompatia furaha kuliko kuwaona wanawake ambao awali walitaka kujiua wakifanya vizuri shuleni na hata kitaaluma.

Makazi hayo yamewawezesha wanawake kuwa wahandisi, viongozi na katika nyanja nyingine kupitia mafunzo wanayopata mjini Addis Ababa, Dessie na vituo vingine.

Msichana huyu aliyepitia masahibu haya kwa sasa ni mkufunzi na ana cheo cha meneja.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles